Serikali ya Somalia inasema washukiwa 18 walihudumu katika ofisi za uhamiaji, ushuru na wafanyikazi. Picha: Somalia AG

Somalia imetoa waranti ya kukamatwa kwa maafisa wa ngazi za juu kwa tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Jumla ya washukiwa 18, wakiwemo wanaohudumu katika utawala wa sasa, wamepangwa kufunguliwa mashtaka, Mwanasheria Mkuu Suleiman Mohamed alisema katika hotuba yake ya televisheni siku ya Alhamisi.

"Baada ya kukamilika kwa upelelezi ulioanza Aprili, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewasilisha majina 18 kwa mahakama kuu ya nchi kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka, 9 tumewatia mbaroni. " Mohamed alisema.

Washukiwa tisa kati ya hao waliotajwa, wametoroka nchini. Wengi wao walihudumu katika ofisi za uhamiaji, Ukusanyaji Ushuru na Kazi, aliongeza.

Wengi zaidi kukamatwa

"Watakabiliwa na mashtaka ya ufisadi, kughushi na ubadhirifu wa fedha za umma, jambo ambalo ni kinyume na sheria zetu," Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema, akifichua uchunguzi zaidi ulikuwa ukiendelea kwa washukiwa zaidi.

Tangazo hilo linakuja miezi miwili tu baada ya Baraza la Mawaziri la Somalia kupitisha hatua kadhaa za kupambana na rushwa, ikiwa ni pamoja na kupitia upya mfumo wa ukaguzi na kufanya mchakato wa ununuzi wa umma kuwa mkali zaidi.

"Kukabiliana na rushwa sio tu ni jambo la lazima la kimaadili lakini pia ni sharti la maendeleo endelevu na Somalia yenye haki na usawa. Tumedhamiria kujenga mifumo ya uwazi na ya uwajibikaji inayohudumia watu wa Somalia,” Rais Hassan Sheikh Mohamud alisema tarehe 11 Mei.

TRT Afrika