Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akiwa katika mkutano na wanahabari mjini Mogadishu. / Picha: Reuters

Somalia inaituhumu Ethiopia kwa kusambaza silaha katika eneo la kaskazini la Puntland, ambalo limejitangazia kujitawala.

Nchi hizo mbili zimekuwa kwenye uhasama wa muda sasa.

Uhasama huo uliongezeka zaidi Januari mosi mwaka huu, baada ya Somaliland kuipa Ethiopia uwezo wa kuifikia bahari nyekundu.

"Somalia imechukizwa na uingizwaji wa silaha katika eneo la Puntland ambao umefanywa na Ethiopia, huku ni kutudharau na kutishia usalama wa kikanda," ilisema Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo katika ukurasa wake wa X, siku ya Ijumaa.

"Tunataka suala hili lisitishwe mapema iwezekanavyo na kutoa wito kwa wadau wa kimataifa kuunga mkono jitihada za kutafuta amani katika Pembe ya Afrika."

Somaliland inapatikana katikati ya mpaka wa Ethiopia na Puntland.

'Usafirishaji silaha'

Katika ukurasa wake wa X, Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia ilisema: "Ushahidi unaonesha kuwa malori mawili yaliyosheheni silaha yakiwasili Puntland kutoka Ethiopia, bila kuwepo makubaliano yoyote ya kidiplomasia."

"Tukio hilo ni dharau kubwa kwa uhuru wa kujitawala wa Somalia na una hatarisha, sio tu usalama wa nchi, bali wa kanda nzima."

Hata hivyo, haikuweka wazi ni lini silaha hizo ziliwasili na nani alikuwa mpokeaji wa shehena hiyo.

Somaliland ilikubali kukodisha sehemu ya eneo la pwani yake, ambalo ni kama kilomita 20 kwa Ethiopia kwa kipindi cha miaka 50, huku Ethiopia ikilenga kuanzisha kambi ya jeshi la wanamaji na bandari katika eneo hilo.

Kutambulika rasmi

Kwa upande wake, Somaliland ambayo bado haitambuliwi na Mogadishu - imesema kuwa Ethiopia itakuwa nchi ya kwanza duniani kuitambua, japo madai hayo bado hayajathibitishwa na Addis Ababa.

Maofisa waandamizi wa Mogadishu wamesema kuwa mkataba unamaanisha kuwa maelfu wa wanajeshi wa Ethiopia waliokuwa Somalia kupambana na Al-Shabaab watahitajika kuondoka eneo hilo.

Wanajeshi hao wametumwa katika ardhi ya Somalia chini ya makubaliano ya pande mbili na makubaliano na Umoja wa Afrika.

Tarehe 14 Agosti Mogadishu ilitia saini mkataba wa kijeshi na mpinzani wa Ethiopia Misri, ambayo imejitolea kujiunga na kikosi cha AU nchini Somalia mwaka 2025.

TRT Afrika