Mlipuaji wakujitoa mhanga anadaiwa kujilipua alipokimbizwa na polisi / Picha : TRT Afrika

Mlipuko umetokea katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu Jumanne asubuhi.

Shirika la habari la SNTV liliripoti katika mtandao wake wa X, zamani twitter kuwa ''Mlipuko mbaya watikisa makao makuu ya Utawala wa Mkoa wa Banadir ya Mogadishu!''

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa mlipuko ulitokea kwenye ukuta wa nyuma wa jengo hilo, na kusababisha uharibifu mkubwa na majeraha mengi. Mamlaka zinajibu kwa haraka iwezekanavyo huku wakiomba utulivu katika kuwahudumia walioathirika.

Baadaye shirika hilo lilichapisha kuwa polisi wamethibitisha kuuawa kwa watu watatu huku wengine wakijeruhiwa katika mlipuko huo.

Idara ya polisi imenukuliwa kusema kuwa mtu aliyevalia fulana ya bomu ya kujitoa mhanga alijilipua kwenye duka la kahawa katika wilaya ya Hamarweyne ya Mogadishu na kuua watu watatu wakati vikosi vya usalama vilipokuwa vikimkimbiza.

Hakuna aliyedai kuhusika na shambulio hilo hadi sasa.

TRT Afrika