"Tumeamua kuwaalika Jamhuri ya Argentina, Jamhuri ya Arabuni ya Misri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ufalme wa Saudi Arabia, na Falme za Kiarabu, kuwa wanachama kamili wa BRICS. Uwanachama utaanza kutumika tarehe moja Januari 2024," Ramaphosa alisema katika mkutano huko Johannesburg.
Wito wa kuongeza ukubwa wa BRICS - Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini - ulitawala ajenda katika mkutano wake wa siku tatu na kuonyesha mgawanyiko ndani ya kundi hilo kuhusu kasi na vigezo vya kuwaalika wanachama wapya.
Lakini kikundi hicho, ambacho hufanya maamuzi kwa kauli ya pamoja, kilikubaliana juu ya "kanuni za mwongozo, viwango, vigezo, na taratibu za mchakato wa upanuzi wa BRICS," alisema Ramaphosa.
Mpangilio mpya wa dunia
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva alisema nia ya nchi nyingine kujiunga na shirika la BRICS ilionyesha jinsi juhudi zake za kutafuta mpangilio mpya wa kiuchumi duniani zilivyo muhimu.
"Tutaendelea kuwa wazi kwa wagombea wapya," Lula alisema katika mkutano wa habari uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisifu tangazo Alhamisi kwamba nchi yake itakuwa miongoni mwa wanachama sita wapya wa klabu ya BRICS ya mataifa yanayoibuka.
"Ni wakati mzuri kwa Ethiopia kwa kuwa viongozi wa BRICS wameidhinisha uanachama wetu katika kundi hili leo. Ethiopia iko tayari kushirikiana na wote kwa ajili ya mpangilio wa dunia wenye kuingiza na mafanikio," Abiy alisema kwenye X, iliyokuwa inajulikana hapo awali kama Twitter.
'Maendeleo ya kihistoria'
Mshauri mkuu wa rais wa Iran alishangilia uamuzi huo kama ushindi wa diplomasia kwa jamhuri hiyo ya Kiislamu.
"Uanachama wa kudumu katika kundi la uchumi unaoinuka kimataifa unachukuliwa kama maendeleo ya kihistoria na mafanikio ya kimkakati kwa sera za kigeni za jamhuri ya Kiislamu," Mohammad Jamshidi aliandika kwenye X.
Takribani nchi ishirini na mbili ziliomba rasmi kujiunga na klabu hiyo, ambayo inawakilisha robo ya uchumi wa dunia na zaidi ya watu bilioni tatu.
Viongozi wengine takriban 50 wa nchi na serikali wanahudhuria mkutano huo huko Johannesburg, ambao unamalizika leo Alhamisi.