Sienna Dutkowski ameongeza thamani katika huduma yake . Picha: Sienna Dutkowski 

Na

Pauline Odhiambo

Iwe simulizi za kutunga ama ala, hadithi za wanawake katika ushujaa bado zinabeba upekee wake.

Katika himaya ya kufikirika ya Wakanda, malaika waliibua mshtuko kwa ujasiri wa kulinda ardhi na watu wao kwa juhudi na maarifa.

Bara la Afrika pia, limekuwa na mashujaa wake wa kike. Takribani miaka 300 kutoka karne ya 17, kikosi kinachoundwa na wanawake cha Agojie, kwa ujasiri mkubwa, kililinda himaya ya Dahomey, ambayo kwa sasa inajulikana kama Benin.

Wakati wa zama zake, kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, alijivunia uwepo wa walinzi wake wakike waliyemlinda hadi mauaji yake ya mwaka 2011.

Licha ya historia ya hali kama hii, wanawake katika tasnia ya usalama ya kisasa hawakubaliki sana na wanakabiliwa na changamoto nyingi katika kuendeleza taaluma zao.

Hili ndilo hasa lililomsukuma Sienna Dutkowski kuanzisha Lady Askari, kampuni ya ulinzi inayolenga wanawake iliyoanzishwa nchini Kenya na Ethiopia ili kuonesha nafasi na jukumu la wanawake katika sekta hiyo.

"Wataalamu wengi wa usalama wako makini kuongeza thamani katika biashara ya ulinzi, kwa kutumia uzoefu wao. Ila wameshindwa kufanya hivyo baada ya kukosa nafasi," Sienna anaiambia TRT Afrika.

Takwimu iliyokusanywa na taasisi ya usalama wa kimataifa ya ISTA, inaonesha kuwa wanawake huunda asilimia 11 ya wafanyakazi katika makampuni binafsi ya ulinzi duniani.

Aslimia 11 ya wafanyakazi katika kampuni binafsi za ulinzi huundwa na wanawake. Picha: Lady Askari

Lady Askari inalenga kuwezesha fursa za mafunzo kwa wataalamu wa usalama, hasa wanawake, ili kuboresha ujuzi wao.

Ulinzi wa karibu

Kwa tafsiri ya haraharaka, Askari ni mtu ambaye anahusika na mambo ya ulinzi.

Askari wengi ncini Kenya hawana uzoefu, jambo linalochangia uwepo mdogo wa walinzi wa kike wachache katika sekta ya ulinzi na usalama.

"Iwapo asilimia 89 ya wafanyakazi wote katika sekta ya ulinzi ni wanaume, hivyo maamuzi yote hutolewa katika mrengo wa mfumo dume," anasema Sienna, ambaye ameajiri watu 97, huku 58 wakiwa ni wanawake.

"Usalama unaolengwa na wanawake haukusudiwi kutofautisha mitazamo ya wanaume dhidi ya wanawake. Inakusudiwa kuchunguza jinsi vipengele kama silika ya akina mama, angavu ya kike na uwezo wa asili wa wanawake kuchanganyika katika mazingira tofauti ya kijamii vinaweza kuwa na thamani katika usalama."

Utafiti wa ISTA unaonesha kuwa watu wengi hudhani kuwa maofisa usalama lazima lazima wawe wanyanyua vitu vizito na kwamba kazi hiyo ni "hatari sana" kufanywa na wanawake.

Sienna anasema kuwa dhana za namna hii humsaidia sana, hasa wakati wa kuandaa timu za ulinzi.

"Kati ya maafisa wetu bora wa ulinzi ni mwanamke mwenye kimo cha futi 5," anasema Sienna.

Dhana ya walinzi wanawake bado ni kitu kipya sana kwa watu wengi./Lady Askari.

Ulinzi wa karibu ni utoaji wa usalama wa kibinafsi ili kuhakikisha watu wa maarufu wanapata ulinzi wenye thamani.

Je, kimo na jinsi ni vigezo kwa walinzi binafsi? Winnie Bolo, askari mwenye kimo cha futi 5, alisomea saikolojia Chuo Kikuu, amefanya kazi na Lady Askari tangu kilipoanzishwa mwaka wa 2020.

"Wazo la kuwa na walinzi wanawake limeshangaza watu wengi. Huwa nafananishwa na katibu muhtasi au msaidizi binafsi na hivyo kufanikisha majukumu yangu kwa ufanisi zaidi. Huwa najichanganya kwenye umati wa watu na hivyo kupata taarifa muhimu kwa urahisi bila kujulikana," anaelezea.

"Si kazi zote za ulinzi zenye kuhitaji nguvu za misuli, ni akili zaidi," ," anasema.

Ujuzi

Mbali na tathmini ya hatari, Lady Askari huwaleta pamoja wataalamu wa usalama wa fani mbalimbali waliofunzwa katika nyanja tofauti za usalama, ikiwa ni pamoja na usimamizi salama wa safari, uchunguzi, kukusanya taarifa za kijasusi, uhalifu, kuzuia hasara na ufuatiliaji wa CCTV.

Uzoefu wa Siena katika usimamizi wa masuala ya usalama umemuwezesha kusimamia kampuni hiyo vizuri, akisaidiwa na mume wake James, ambaye ana uzoefu wa miaka 20 katika nyanja ya ulinzi wa baharini.

Kigezo cha kimo kinaweza kutumika vizuri katika masuala ya usalama. Picha: Lady Askari

Anakumbuka namna mumewe alivyotambua thamani ya wanawake katika ulinzi wakati akisimamia timu inayomlinda balozi wa kike wakati wa misheni nchini Iraq.

"Balozi alimuuliza James kuwa ni kitu gani kingetokea iwapo angehitaji kutumia huduma ya maliwato. Akamjibu kuwa timu hiyo ya ulinzi ilikuwa imebaini eneo maalumu ambalo angetumia balozi huyo," Sienna anasimulia.

Balozi alijibu kwa kuashiria kwamba James atahitaji kuhamasisha timu yake ya usalama ya wanaume wote kusafisha bafu. Kisha ingemlazimu kumweka mtu karibu na mlango na mwingine karibu na dirisha huku balozi akitumia chumba hicho.

"Walinzi wa kike wangekuwa na uwezekano wa kuchanganyikana vyema na pengine kuwa waangalifu zaidi katika hali hiyo," anasema Sienna.

"Ikiwa lengo kuu ni kuunda suluhu bora zaidi za usalama kwa wateja wote, lazima tuzingatie ujuzi zaidi. Kuwa na wataalam wanawake kuna manufaa kwa njia nyingi, na hii ni sehemu ya sababu tulichagua jina la aina hii kwa shirika letu. "

Ushirikiano wa kupeana taarifa

Kikundi cha Lady Askari kinajumuisha wanawake pekee - jambo ambalo Sienna anasema ni zuri kwa kampuni hiyo.

"Dhana kuwa wanawake ni watu wa kupenda tabia za umbea ni ya muhimu sana hasa katika masuala ya uchunguzi," anasema. "Katika dunia ya ulinzi na usalama, suala la kupeana taarifa ni la muhimu sana."

Lady Askari huwaleta pamoja wataalamu wa ulinzi wenye uzoefu tofauti.Picha: Lady Askari

Uzoefu wa Sienna katika maendeleo ya jamii imemsaidia kufanya kazi na mashirika mbalimbali ya ndani na kimataifa ili kuimarisha usalama wa jamii.

"Tunafanya kazi na mashirika kama vile I Am My Bodyguard, ambayo hufanya mafunzo ya usalama wa kibinafsi kwa watoto," anasema. "She Hacks' na Protect Us Kids Foundation ni miongoni mwa mashirika mengine ambayo tumeshirikiana nayo kuandaa programu za ulinzi wa watoto kwa watoto, haswa katika kuangazia tovuti za mitandao yenye kuathiri watoto."

Lady Askari pia imejenga viwanja kadhaa vya michezo katika magereza kote nchini Kenya ili kutenga maeneo salama ambapo watoto wa akina mama waliofungwa wanaweza kucheza.

Sienna sasa anafanya kazi ya kuajiri dereva wa kike aliye na uzoefu kama mekanika, hata kampuni inapochunguza fursa zaidi za mafunzo kwa wafanyakazi wa Lady Askari.

"Tunatoa mafunzo ya udereva ili kuongeza ujuzi wa watu kwa upande wa usalama, jambo ambalo linahusiana kwa karibu na udereva wa kujihami," anaiambia TRT Afrika.

"Changamoto katika hili ni kwamba udereva wa kujihami unahitaji njia maalum na leseni fulani ya mafunzo. Tunalenga kushirikiana na shule ya udereva inayoheshimika ili kufanikisha hili."

TRT Afrika