Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) imeanza kusikiliza kesi zake baada ya kusitisha shughuli hiyo kwa muda wa miezi minne.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa EACJ, mahakama jumla ya kesi 25, zitasikilizwa katika vikao vya mahakama hiyo ambavyo vitadumu hadi Oktoba 11, 2024.
"Mahakama ililazimika kusitisha shughuli zake za mwezi Mei na Juni kutokana na uhaba wa fedha. Hali hii imechangia ongezeko kubwa la kesi ambapo kwa sasa mashauri yamefikia zaidi ya 260. EACJ inaendelea na jitihada za kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu suala hili," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kulingana na EACJ, changamoto hiyo ya kifedha inatatiza shughuli za utoaji haki ambayo ni moja ya majukumu ya mahakama hiyo.
EACJ ilianzishwa mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kuhakikisha kuwa sheria zote ndani ya nchi wanachama zinatafsiriwa kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
Pia hutoa maoni na ushauri wa kisheria, pamoja na kujihusisha kwenye usuluhishi.