Shirika la WFP limesema kuwa linarejesha operesheni zake nchini Sudan. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa lililazimika kusimamisha shughuli zake katika nchi hiyo inayokumbwa na ghasia, wiki mbili zilizopita baada ya wafanyakazi wake watatu kuuawa.
Siku ya Jumatatu tarehe 1 Mei, Mkurugenzi Mkuu wa WFP, Cindy McCain aliandika katika mtandao wa Twitter, ‘’ Kwa kuwa mzozo wa Sudan unasababisha mamilioni ya watu kukumbwa na njaa, WFP imeamua kubadilisha uamuzi wake wa kusimamisha kwa muda shughuli za misaada, kutokana na vifo vya wafanyakazi wake.’’
Cindy McCain amesema kuwa shirika hilo ‘’linarudisha misaada haraka’’ ili kuweza kutoa usaidizi wa dharura unaohitajika na wengi kwa sasa.
Wafanyakazi hao wa WFP waliuawa wakati vita vilipoanza kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha Kijeshi cha Msaada wa Haraka, RSF.
Wakati huo huo kiongozi wa misaada wa UN anasafiri kwenda Sudan kutokana na 'kuzorota kwa hali ya kibinadamu’ katika taifa hilo lililotumbukia katika mzozo, ametangaza katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Tangazo hilo la katibu mkuu Antonio Guterres la Jumapili, limekuja muda mfupi baada ya vikosi hasimu nchini Sudan kutangaza kuongezwa kwa muda wa kusitisha mapigano licha ya kuwa wote wamekiuka makubaliano hayo huku mashambulio yakielekea katika mji mkuu wa Khartoum.
Mapigano hayo ni kati ya vikosi vinavyo mtii kiongozi wa jeshi la taifa Abdel Fattah al-Burhan dhidi ya naibu wake wa zamani Mohammed Hamdan Dagalo anayeamrisha kikosi cha RSF, kinachoaminiwa kumiliki silaha kali.
Zaidi ya watu mia tano wameuawa na makumi ya maelfu wengine kulazimika kukimbia makwao tangu ghasia kuzuka Aprili 15.
‘’Kiwango na kasi ya hali inavyozorota haijawahi kuonekana nchini Sudan. Tuna wasiwasi mkubwa wa athari za hivi karibuni na za muda mrefu zitakazowakumba raia wa nchi hiyo pamoja na nchi jirani,’’ aliongeza msemaji wa Katibu Mkuu wa UN, Stephane Dujarric.
Aliongeza kuwa UN inamtuma ‘’mara moja’’ Martin Griffiths, mratibu wake wa misaada ya dharura nchini humo ‘’ kufuatia kuzorota kwa kasi kwa hali ya kibinadamu.
Juhudi za kutafuta makubaliano katika mzozo huo wa Sudan zimeshindikana mpaka sasa.