Vikosi vya usalama nchini Somalia vimesema kuwa shambulizi la anga la hivi karibuni, limefanikiwa kuwauwa zaidi ya wapiganaji 13 wa vikundi vya Daesh na ISIS, katika eneo la Bari.
Katika taarifa yake iliyotolewa siku ya Jumatatu, shambulio hilo lililenga magaidi hao waliokuwa wamejificha, katika muendelezo wa mapambano dhidi ya wapiganaji, kulingana na maofisa wa usalama.
“Operesheni hiyo ilidumu kwa saa 24 na kufanikiwa kuua zaidi ya wapiganaji 13 katika eneo la Dhasaq, liliokuwa katika safu ya milima ya Calmiskaad,” kitengo cha kupambana na ugaidi cha Puntland kilisema siku ya Jumatatu.
Maofisa wa usalama pia wameendelea na operesheni zaidi katika eneo la Hararyo na Toga-Jeceel, hadi kuelekea kwenye ngome za Daesh/ISIS.
“Walifanikiwa kubaini ngome zilizokuwa zikitumika na vikundi vya kigaidi vya ISIS,” kilisema kitengo hicho kupitia taarifa yake kwenye ukurasa wa X.
Hata hivyo, vikosi hivyo vya usalama havikuweka wazi ni nchi gani iliyotekeleza shambulio hilo la anga.
Shambulio hilo linakuja zaidi ya wiki moja baada ya Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani (AFRICOM) kuthibitisha kutekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya ISIS na Somalia.