Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya imeamuru kusimamishwa kwa muda kwa programu ya kutuma ujumbe kwa Telegram kote nchini.
Mamlaka hiyo imeagiza kampuni za mawasiliano za Safaricom, Airtel na Jamii telkom, zinazosambaza mtandao wa mawasiliano nchini kuzimia data Telegram kuanzia kuanzia saa 7:00 asubuhi hadi 10:00 a.m. na 1:00 p.m. hadi 4:00 p.m, Jumatatu hadi Ijumaa, hadi Novemba 22.
Katika barua iliyotumwa kwa watoa huduma za mtandao, Mamlaka ya Mawasiliano iliamuru kuwa watoa huduma wote wa simu, kusimamisha upatikanaji wa Telegram kwa saa walizotaja kuwa muhimu kwa mtihani.
Uamuzi huo unajiri huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu matumizi ya Telegram katika kuwezesha shughuli haramu, ikiwa ni pamoja na kushiriki maswali ya mitihani na majibu wakati wa mitihani inayoendelea ya Kitaifa ya Sekondari Kenya (KCSE).
Hii si mara ya kwanza kwa Wakenya kukumbana na masuala ya upatikanaji wa Telegram wakati wa mitihani ya KCSE. Mnamo Novemba 2023, usumbufu kama huo uliripotiwa, na kama mwaka huu, kukatika kwa mtandao huo kulihusu mitandao ya Safaricom pekee.
Huku serikali ikisisitiza kuwa hii ni hatua ya lazima ili kulinda uaminifu wa mitihani ya KCSE, uamuzi huo umezua hasira na malalamiko miongoni mwa wafanyabiashara na wasimamizi wa mitandao ya kijamii wanaotegemea Telegram kwa mauzo yao na mawasiliano.