Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Sasa ni rasmi kuwa Bassirou Diomaye Faye ndiye Rais mteule mwenye umri mdogo kabisa barani Afrika, akiwa na miaka 44.
Licha ya kwamba kiongozi wa mpito wa Mali, Assimi Goïta na mwenzake kutoka Burkina Faso, Ibrahim Traoré ni wadogo kiumri kuliko Faye, wawili hao hawakuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia kama ilivyo kwa mtoza ushuru huyo wa zamani kutoka mamlaka ya kodi nchini Senegal.
Safari ya Faye, ambaye hana uzoefu wowote kisiasa kufikia hatamu ya uongozi wa juu kabisa nchini humo haikuwa rahisi, hasa ukizingatia alikuwa ametoka kutumikia kifungo cha zaidi ya miezi 11 jela.
Wakati wafuasi wake wakiendelea kusheherekea ushindi huku wakisubiria kwa shauku, mchakato wa utangazaji matokeo rasmi ambao unatazimwa kuanza Aprili 3, Faye amedhamiria kuongeza uwazi atakapokuwa madarakani na kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya rushwa.
“Naahidi kupambana na rushwa katika ngazi zote huku nikilenga kufufua baadhi ya taasisi ndani ya nchi yetu,” amesema mwanasiasa huyo kijana, ambaye pia yuko tayari kubadili Katiba na kupunguza mamlaka ya Rais.
Ushindi wa kishindo wa rais Bassirou Diomaye Faye nchini Senegal ni mfano wa kushangaza. Akiwa na umri wa miaka 44 pekee, Faye anakuwa sio tu Rais mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya nchi hiyo, bali Afrika kwa ujumla, huku akionekana kuungwa zaidi mkono na makundi makubwa ya vijana na watu waliokata tamaa.
Ni wazi kuwa ushindi wake unawakilisha mabadiliko makubwa katika hali ya kisiasa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Kulingana na Zitto Kabwe, kiongozi mstaafu cha Chama cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, ushindi wa Faye unadhihirisha wazi kuwa mategemeo ya bara zima la Afrika sasa yapo kwenye damu changa za vijana.
Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini, ambaye pia alikuwa sehemu ya ujumbe wa wasimamizi wa uchaguzi wa Rais nchini Senegal, chini ya mwamvuli wa Pan African Solidarity Network of Opposition Leaders, amesema kuwa huu ni mwenendo mpya ambao unapaswa kutupiwa jicho, katika vuguvugu la kisiasa linaloendelea katika ukanda huo wa bara la Afrika.
"Ni dhahiri kuwa watu wamechoka na kuchoshwa na hali duni za maisha ambayo ni matokeo ya tawala za muda mrefu na hivyo kuamua kuchagua damu changa," anaiambia TRT Afrika.
Anasema kuwa ushindi wa Faye ni kiashiria cha bara la Afrika kuwa tayari kupisha tawala za watu wenye umri mdogo lakini wenye fikra na maono makubwa kwa manufaa ya watu wao.
Zitto anaweka wazi kuwa Senegal imetoa mfano mzuri wa mabadiliko ya Kidemokrasia kwa nchi nyingi za Afrika, inayodhihirisha ustahimilivu wake katika demokrasia.
"Hiki ni kiashiria kizuri kuwa sasa Afrika iko tayari kuwapa nafasi vijana, tumeona Burkina Faso, Mali na sasa ni Senegal, hatujui nchi gani nyingine itafuata," anaongeza.
Kulingana na Jukwaa la Kiuchumi Duniani, Afrika ni bara changa zaidi kwa idadi ya watu, lakini uongozi wake bado unatawaliwa na watu wenye umri mkubwa.
Jukwaa hilo, pia linadai kwamba Umoja wa Afrika ndio sehemu pekee yenye kuhakikisha serikali za kitaifa zinajitolea kwa uwakilishi wa vijana. Hata hivyo, ukosefu wa ushiriki wa kutosha wa kisiasa kwa vijana wa Kiafrika unatishia muundo wa asasi za kiraia.
Kwa upande wake, Christian Gideon mtafiti na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi kutoka Mwanza, Tanzania anasema kuwa ushindi wa Faye ni ishara kuwa ni wakati muafaka kuondoa vifungu tata kwenye katiba ambavyo vinawaondolea vijana sifa za uongozi.
"Tubadili fikra za kuweza kuwafasiri vijana, Afrika inabidi ianze kuwaamini vijana, bahati mbaya sana wazee ndio wameongoza bara hili na matokeo yake yanaendelea hadi leo hii huku wengi wakishindwa kuongoza nchi zao vizuri," anaeleza Gideon.
Mchambuzi huyo anaamini kuwa Faye ndiye tumaini jipya la Senegal, na ni wakati muafaka kwa bara la Afrika kubadilika ili lipate fikra za vijana, kwani wana nguvu na wanakuja na mawazo na fikra mpya.
"Ukimsikia tu Faye anavyozungumza, moja kwa moja utakubaliana nami kuwa yeye ndio tumaini jipya la bara hili," anasema.
Ni imani ya Gideon kuwa imani kwa vijana katika masuala ya uongozi itaondoa unafiki mkubwa ulioghubika nyanja za kisiasa barani Afrika.
Hata hivyo, Gideon ana imani kuwa ushindi wa Faye, utakuwa chachu kubwa kwa vijana wengi wa Afrika katika kuifikia safari ya mabadiliko.
"Faye amewajengea vijana wengi wa Afrika moyo wa uthubutu, naamini watatoka mafichoni na kujaribu bahati zao," anaongeza.