Shirika la Afya Duniani , WHO linasema ripoti za vikosi kuvamia vituo vya afya na kuvipora nchini Sudan zinatia wasiwasi sana.
"Ukosefu wa upatikanaji salama wa chakula, umeme, maji, wafanyakazi na upungufu wa vifaa vya matibabu unafanya vituo vingi vya afya kukosa kutoa huduma wakati ambapo kuna maelfu ya majeruhi wanaohitaji huduma ya haraka," Dkt. Tedros Adhanom Mkurugenzi mkuu wa WHO amesema katika mtandao wa twitter.
Dkt. Adhanom ameongezea kuwa takribani watu 300 wamekufa na zaidi ya watu 3000 kujeruhiwa katika vita hivi vilivyoanza kati ya vikundi vya majeshi nchini Sudan tangu tarehe 15 Aprili.
Siku ya Jumatano, Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan ilisema katika taarifa kuwa ni hospitali 39 tu kati ya 59 jijini Khartoum zinafanya kazi kikamilifu.
Inasema hospitali 9 zilishambuliwa kwa mabomu na 16 zililazimika kuhamishwa kwa nguvu.
" Tunaomba pande zote za mgogoro zihakikishe kuwa vituo vya afya ikiwa ni pamoja na zahanati na hospitali na ambulensi zinalindwa na wahudumu wa afya wasilengwe kamwe," Ghazali Babiker mwakilishi wa shirika la kimataifa la madakitari la ‘Doctors without Borders’ nchini Sudan.
Shirika la Umoja wa mataifa ya linalohusika na idadi ya watu ,UNFPA ,linasema lina wasiwasi kuhusu takwimu za wanawake wajawazito 219,000 katika jiji la Khartoum, ikiwa ni pamoja na 24,000 ambao wanatarajiwa watajifungua katika wiki zijazo na huenda hawataweza kupata huduma za afya.