Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini Rwanda maarufu Rwanda FDA imetangaza kupiga marufuku bidhaa za urembo zaidi ya 130 zikiwemo mafuta ya mwili, sabuni na krimu kwa madai ya kuwa zina kemikali inayohatarisha afya.
"Rwanda FDA inachapisha Orodha ya Vipodozi vilivyokataliwa katika soko la Rwanda. Bidhaa yoyote ya urembo ikiwemo isiyoorodheshwa, lakini yenye moja au zaidi ya viungo viliyokatazwa (kiwango cha juu cha matumizi) pia ni marufuku kwenye soko la Rwanda. Waigizaji na wasambazaji wote wanaonywa kutekeleza," taarifa ya Rwanda FDA ilisema.
Kulingana na orodha iliyotolewa, bidhaa zilizotajwa zinajumuisha vipodozi vyenye viungo vya kugeuza ngozi rangi kuwa nyeupe na kemikali kama vile hydroquinone, asidi ya kojic, steroids na kemikali aina ya zebaki.
Miongoni mwa vipodozi vilivyotajwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na Fair &White/so white, Miss White /Fair & White, Maxi White, Caro Light, Teint Jaune/ Lait Clarifiant, éclair 600, na Extra Clair-Lightening.
Mnamo 2019, Sudan Kusini pia iliweka marufuku ya uuzaji wa krimu za kujichubua na baadhi ya vipodozi vyenye madhara.
Mnamo 2019, Bunge la Afrika Mashariki lilipitisha azimio lililotaka kuwepo kwa marufuku ya kikanda dhidi ya uagizaji na utengenezaji wa bidhaa zenye kemikali aina ya hydroquinone.
Angalau nchi 10 za bara la Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Kenya, Côte D'ivoire, Ghana, Uganda, Tanzania, Rwanda, Nigeria, Cameron na Sudan Kusini zimepitisha kanuni za kudhibiti krimu za ngozi zenye sumu. Tangu 2015, nchi nane zimechukua hatua za kuzuia vipodozi hivyo vyenye sumu.