Rais Ruto anasisitiza kuwa sheria mpya ya fedha itasaidia Kenya kutoka kwa utegemezi wa madeni ya nje. Picha : Reuters

“Nchi inajengwa na kodi, na nchi inajengwa na ushuru, haijengwi na madeni. Hapo ndio tuko."

Maneno ya kutia moyo kutoka kwa Rais William Ruto wa Kenya, wakati taifa linalalamikia gharama kubwa ya maisha na kodi ya juu zaidi kuwahi kutozwa.

Rais Ruto alikuwa akizungumza wakati wa ibada ya pamoja ya madhehebu mbalimbali iliyoandaliwa katika ikulu ya Sagana iliyoko Kaunti ya Nyeri nje kidogo ya mji mkuu Nairobi.

Rais huyo amesema kuwa utawala wake umeweza kuleta utulivu wa uchumi licha ya ukosoaji kutoka kwa wapinzani wake kwamba hali ya uchumi imekuwa mbaya wakati wa utawala wake.

Viongozi wa upinzani wakiongozwa na kinara Raila Odinga wamekuwa wakishinikiza wananchi kufanya maandamano kulalamikia gharama ya juu ya maisha.

Maandamano hayo yameishia kila mara na uharibufu wa mali ya umma, uporajina wakati mwingine vifo.

Viongozi wa upinzani wakiongozwa na kinara Raila Odinga wamekuwa wakishinikiza wananchi kufanya maandamano kulalamikia gharama ya juu ya maisha. Picha : Reuters 

Hali hii ilitokana na sheria ya fedha iliyopitishwa bungeni inayolenga kuwatoza wafanyakazi nchinihumo kodi za juu pamoja na kodi mpyakama vile ya nyumba za watu wa pato la chini.

Upinzani uliwasilisha kesi mahakamani kutaka sheria hiyo isimamishwe kutumika, japo mwishoni mwa mwezi Julai, mahakama iliidhinisha sheria hiyo.

Rais Ruto anasisitiza kuwa sheria hii itasaidia Kenya kutoka kwa utegemezi wa madeni ya nje.

Ameongeza kuwa tayari nchi iko katika mkondo wa kulipa madeni yake mapema.

"Tuna deni kubwa la thamani ya dola bilioni 2 na inabidi tuanze kulipa ifikapo Juni mwaka ujao. Hatutasubiri hadi hapo.'' Alisema Rais Ruto. ''Hayo mashirika ya kitapeli ya kukadiria mikopo, yale yanayotumika kuongeza riba ya deni sasa yametuandikia barua yakihoji ni kwa nini tunalipa mkopo huo mapema,” aliongeza.

Kwa mujibu wa takwimu za fedha za serikali, kiasi kikubwa cha pato la kitaifa na deni la nchi kinatoka ndani ya nchi.

Ruto anasema kuwa, bila kuchukua hatua za dharura kulipa deni hilo, Kenya ingetishia kushindwa kulipa deni lake.

Vuta nikuvute kati ya serikali ya Ruto na upinzani bado unaendelea huku pande zote mbili zikisema kuwa ziko tayari kufanya mazungumzo kuepuka marudio ya maandamano yaliyoishia kwa ghasia. Hijabainika kikao hiki kitafanyika lini na pia hawajakubaliana mada kuu za kujadili.

TRT Afrika