Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki (EAC) wamekubaliana kupeleka mgombea mmoja kuwania nafasi ya uenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, utakaofanyika baadaye mwakani, amebainisha Rais wa Kenya, William Ruto.
Kiongozi huyo, aliyekuwa anahutubia wajumbe kutoka Bunge la Afrika Mashariki(EALA) wakati wa ufunguzi wa wa Mkutano wa 3, kikao cha 2 jijini Nairobi, amegusia kwamba yeye na viongozi wenzake wameshakutana na kukubaliana kupeleka jina la mgombea mmoja ili kumrithi Moussa Faki Mahamat, ambaye nafasi yake ndani ya Tume ya Umoja wa Afrika(AUC) inafikia kikomo mwaka huu.
"Tumekaa pamoja na kushauriana kama wakuu wa nchi za EAC na kukubaliana kuwa ni vyema tumuunge mkono mgombea mmoja, hii inaonesha nguvu na umoja wetu ndani ya Jumuiya yetu," amesema Rais Ruto.
Ameongeza: Ishara hii inadhihirisha nguvu yetu kama Jumuiya.
Kauli ya Rais Ruto inakuja baada ya Kiongozi Mkuu wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga kuonesha nia ya kuwania nafasi hiyo, na kuungwa mkono na baadhi ya viongozi akiwemo Ruto mwenyewe, Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo.
Nafasi hiyo kwa sasa ipo chini ya Moussa Faki Mahamat ambae ni raia wa Chad, ambae aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo. Awamu yake ya pili ya uongozi inakwisha mwaka huu 2024.
Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga atalazimika kusubiri hatma ya mapendekezo na mabadiliko katika utaratibu wa kumchagua mrithi wa Moussa anayemaliza muda wake kama mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, baadae mwaka huu. Mabadiliko hayo yanaziondolea sifa nchi wanachama wa AU zilizowahi kushika nafasi za uenyekiti na makamu mwenyekiti, kati ya mwaka 2002 mpaka leo.
Mbali na Kenya, nchi nyingine inayosubiria maamuzi ya wakuu wa AU ni Rwanda, ambayo ilitoa makamu mwenyekiti kwenye umoja huo.
Tume ya Umoja wa Afrika imekuwa na utaratibu wa kupokezana nafasi ya uenyekiti kwa mzunguko kulingana na maamuzi yake ya mwaka 2018, na kwa sasa, zamu ilidondokea katika ukanda wa Afrika Mashariki.