Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeamua kuendelea kutumia asilimia sita kama riba yake kwa robo mwaka, utakaoisha Disemba 2024.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na BOT, siku ya Oktoba 3, 2024, uamuzi huu unatokana na matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kuwa chini ya lengo la nchi la asilimia tano.
Benki hiyo, pia imetabiri ukuaji wa uchumi kwa hali ya kuridhisha, sambamba na kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi duniani na nchini Tanzania.
"Uchumi wa dunia unatarajiwa kuendelea kukua sambamba na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha. Kutokana na hali hii, Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia wanakadiria uchumi wa dunia kukua kwa asilimia 3.2 na asilimia 2.6, mtawalia, mwaka 2024," ilisema taarifa hiyo iliyowekwa kwenye ukurasa wa X.
Kwa mujibu wa BOT, mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kupungua, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi sambamba na kupungua kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan mafuta na mbolea.
"Kutokana na hali hii, benki kuu katika nchi nyingi zinatarajiwa kupunguza au kutokubadili riba zao za sera ya fedha. Vilevile, benki kuu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zinatarajiwa kufuata mwenendo huu wa kisera," taarifa hiyo iliongeza.
BOT pia imeongeza kuwa bei za bidhaa katika soko la dunia zimeendelea na zinatarajiwa kuendelea kuwa tulivu. Katika robo ya mwaka inayoishia Disemba 2024, bei za mafuta ghafi zinatarajiwa kuwa kati ya dola za Marekani 72 hadi 82 kwa pipa, kutokana na ongezeko la uzalishaji.