Mashabiki kutoka Afrika Mashariki hasa Tanzania walifuatilia kwa karibu huku wakitarajia ndugu wawili wanasarakasi maarufu Ramadhan Brothers ambao ni washiriki kutoka nchi hiyo wanaweza kuibuka kidedea.
Ramadhani Brothers, kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii, wamewashukuru mashabiki walioko nchini Marekani na kote duniani kwa kuwapigia kura kadri wawezavyo ili wapate ushindi.
Kupitia ukurasa wao wa Instagram vijana hao walisema, "Habari wadau, matokeo yametangazwa. Hatukukusanya kura za kutosha. Tumeshika nafasi ya tano katika mashindano haya, na tunapenda kuwashukuru AGT kwa fursa na watu wote waliojitokeza kutupigia kura. Mapambano yanaendelea."
Watanzania wengi duniani walipiga kura kwa kutumia njia kama VPN ili waweze kupiga kura kwa ajili yao kwani sheria zinasema kuwa ni watu kutoka nchini Marekani pekee ndio wanaweza kupiga kura kwa ajili ya washiriki wa AGT.
Mmarekani Adrian Stoica na mbwa wake, Hurricane, ndio walishinda AGT kupitia maigizo aliyokuwa akifanya yeye na mbwa wake. Wamemshinda Ramadhani Brothers, Putri Ariani kutoka India, Anna DeGuzman na Murmuration na kupata zawadi ya dola milioni moja na nafasi katika onyesho kuu huko jiji la Las Vegas, Marekani.
Hii ni mara ya kwanza kwa nchi ya Tanzania kushiriki shindano hilo kubwa na la kimataifa ambalo hujumuisha watu kutoka mataifa mbalimbali wenye vipaji tofauti.