Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekutana na Waziri Mkuu wa Libya, na kuangazia masuala mbalimbali yakiwemo uhusiano wa nchi hizo mbili, masuala ya kikanda ikiwemo mashambulizi ya Israeli dhidi ya Palestina.
Erdogan alimpokea Abdulhamid Dbeibah siku ya Ijumaa, katika jumba la Rais lililoko katika mji mkuu wa Uturuki, Ankara, ilisema taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.
Katika kikao chao, Erdogan alisema kuwa Ankara iko tayari kutoa msaada wa kuanzisha majadiliano ya "kuimarisha umoja na mshikamano nchini Libya na kulinda uhalali wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya," inayoongozwa na Dbeibah.
Akibainisha kuwa uhusiano kati ya Uturuki na Libya unaendelea kustawi "katika nyanja zote," taarifa hiyo ilisema Erdogan alisisitiza kwamba kuhusu ushirikiano wa nishati, nchi hizo mbili zinapaswa kuwa na "mawasiliano ya karibu ili kulinda maslahi yao ya pamoja katika eneo la mashariki ya Mediterania."
Dhidi ya vita vya Israeli huko Gaza
Kwa mujibu wa kurugenzi hiyo, Rais wa Uturuki alioneshwa kufurahishwa na kitendo cha Libya kuiunga mkono Palestina.
"Rais Erdogan amesema kuwa ameunga mkono juhudi za Libya kuingilia mashambulizi ya Israeli dhidi ya Palestina katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, kama ilivyo kwa Uturuki," ilisema taarifa hiyo.
Israeli imeendeleza mashambulizi yake ya kinyama katika eneo la Gaza ya Palestina toka shambulizi la Hamas la Oktoba 7, licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kusitisha mashambulizi hayo.
Zaidi ya Wapalestina 36,200 wameuwawa katika eneo la Gaza, wengi wao wakiwa ni akina mama na watoto, na kujeruhi wengine 81,800, kulingana na mamlaka za afya za eneo hilo.
Gaza imesalia kuwa magofu, huku kukiwa na vizuizi katika upatikanaji wa chakula, maji safi na dawa, miezi nane toka kuanza kwa vita hivyo.
Israeli imetuhumiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo katika hukumu yake ya hivi karibuni, ilitakiwa kusitisha operesheni yake katika eneo la Rafah, ambapo zaidi wa Wapalestina milioni moja wanatafuta hifadhi kabla ya eneo hilo kuvamiwa Mei 6.