Rais wa Somalia Hassan Sheikh amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama na kuungana ili kuwatokomeza Khawarij nchini humo.
Rais huyo aliyezungumza wakati wa kikao cha dharura na vyombo vya usalama mjini Mogadishu, alisema kuwa mafanikio ya vita dhidi ya ugaidi yanategemea uungwaji mkono na ushirikiano wa watu wa Somalia.
Serikali ya Somalia imepiga marufuku matumizi ya jina "al-Shabaab," likirejelea kundi la kigaidi lenye uhusiano na al Qaeda ambalo taifa hilo lenye Waislamu wengi lilisema ni dhehebu potovu.
Badala yake , Wizara ya Masuala ya Kidini ya Somalia ilisema linafaa kuitwa "Khawarij," neno linaloelezea madhehebu potovu.
"Ndugu zangu watu wa Somalia, magaidi wa Khawarij hawapendi watu na serikali, na kwao sisi sote ni maadui zao na wana kiu ya damu yetu. Tuungane kwa ajili ya kuwaangamiza, na kuunga mkono Jeshi la Taifa na waambieni wale wanaojificha miongoni mwenu,'' alisema Rais Hassan.
Rais Hassan Sheikh Mohamud, pamoja na Waziri Mkuu Hamsa Abdi Barre, waliongoza kikao cha dharura cha usalama na vyombo vya usalama vya nchi hiyo, ambapo vyombo vya usalama vilitoa taarifa kuhusu shambulio la kigaidi dhidi ya watu wa Somalia katika ufukwe wa Lido.
Pia viongozi hao waliandamana kuwafariji familia za waliopoteza jamaa katika shambulio hilo la Ijumaa jioni.
Watu 32 walithibitishwa kufa na wengine zaidi ya 60 walijeruhiwa katika shambulio linaloaminiwa kufanywa na wanamgambo wa Khawarij.
"Inna Lillahi wa Inna Ileyhi Rajiun. Shambulio la kigaidi katika ufuo wa Lido linaonyesha ukatili wa Khawarij na lengo lao la kuua watu wa Somalia kila mahali. Serikali imejitolea kuangamiza kundi hili kutoka nchi nzima."
Rais aliviagiza vyombo vya usalama vya nchi hiyo kuwa macho zaidi dhidi ya mashambulizi ya kigaidi yanayowadhuru watu wa Somalia.