Rais wa Gabon Ali Bongo "amewekwa katika hali ya kustaafu," mkuu wa walinzi wake wa rais aliliambia gazeti la Le Monde siku ya Jumatano baada ya maafisa wa waasi kusema kuwa wamempindua.
"Amestaafu. Ana haki zake zote. Ni mtu wa kawaida wa Gabon, kama kila mtu," Brice Oligui Nguema alisema, huku akikana kwamba amekuwa kiongozi wa mapinduzi.
Kiongozi wa Walinzi wa Rais alionekana katika kanda ya video iliyorushwa na runinga ya taifa mapema Jumatano akiwa amebebwa juu na mamia ya wanajeshi waliokuwa wakiimba "Rais Oligui."
Alipoulizwa kwa nini Bongo ilibanduliwa, aliliambia gazeti kuwa: "Kulikuwa na hali ya kutoridhika Gabon na zaidi ya kutoridhika huko kulikuwa na mkuu wa nchi ambaye kila mtu analalamika juu yake, lakini hakuna mtu anayefanya chochote."
"Hakuwa na haki ya kugombea muhula wa tatu. Katiba ilikuwa imekanyagwa. Mchakato wa uchaguzi haukuwa sahihi. Kwa hiyo jeshi liliamua kufungua ukurasa na kufanya jambo."
Bongo alipatwa na kiharusi mwaka 2018 ambacho kilimweka kando na maisha ya umma kwa muda wa miezi 10 na kumuacha na matatizo ya kutembea na matatizo ya kuzungumza.
Mamlaka ya uchaguzi nchini Gabon ilikuwa imetangaza mapema Jumatano kwamba Bongo alikuwa ameshinda muhula wa tatu kwa kura 64.27 baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata mwishoni mwa juma.