Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, akiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame./ Picha: AA

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, amesema hana pingamizi lolote kukutana na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Tshisekedi ameelezea msimamo wake kama juhudi za kutatua hali iliyopo Mashariki mwa DRC na kurudisha utulivu katika maeneo hayo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Angola, Teté António, alitoa taarifa hiyo mwishoni mwa Februari kufuatia mkutano kati ya Rais wa Angola, João Lourenço, na rais wa DRC, Félix Tshisekedi, mjini Luanda, Angola.

Rais wa Angola, João Lourenço ambaye ameteuliwa kuwa mpatanishi wa kushughulikia hali ya mashariki mwa DRC na Umoja wa Afrika (AU), alifanya mikutano na viongozi hao; Félix Tshisekedi na Paul Kagame kando ya mkutano wa 37 wa AU uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Lourenço amepewa jukumu la kufanikisha mkutano kati ya viongozi hao wawili ili kuepuka vita vya pande zote kati ya mataifa yao.

Viongozi hao wawili, Félix Tshisekedi na Paul Kagame wamekuwa wakitofautiana juu ya kukithiri mashambulio yanayoaminiwa kufanywa na waasi wa M23 ambayo yamesababisha mauaji ya mamia ya watu na kuwahamisha zaidi ya watu milioni moja mashariki mwa DRC tangu 2021.

TRT Afrika na mashirika ya habari