Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameweka wazi azma ya Serikali yake katika kukuza zao la Karafuu visiwani Zanzibar.
Kulingana na Rais Samia, Tanzania imelenga kuleta wawekezaji za zao hilo ikiwa ni jitihada ya kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao hilo katika soko la dunia.
Akizungumza mara baada ya kuzindua Jengo la Kitega Uchumi la Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Chake Chake kisiwani Pemba, Rais Samia pia amewarai wakulima kuendelea na ukulima wa zao hilo kwa wingi na kwa tija zaidi ili kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo na hatimaye kuinua uchumi wa buluu.
Kwa namna ya pekee, Rais Samia amewataka wakulima wa karafuu kuacha kuchepusha na kuuza kwa magendo zao hilo.
Rai hiyo inakuja baada ya Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi kutembelea bandari ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba na kushuhudia karafuu za magendo tani 9.5, zenye thamani ya pesa za Kitanzania, Milioni 140.
Hali kadhalika, uzinduzi wa Jengo hilo unakuja siku chache kabla ya wananchi wa Zanzibar kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyomuodoa madarakani Sultani wa Zanzibar na serikali yake.