Rais Samia awarai viongozi wa dunia kutumia Kiswahili kukuza utangamano

Rais Samia awarai viongozi wa dunia kutumia Kiswahili kukuza utangamano

Tarehe 7 Julai imetengwa rasmi kama siku ya Kimataifa ya maadhimisho ya lugha ya Kiswahili.
Huu ni mwaka wa tatu wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani baada ya shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni ya Umoja wa Mataifa (UNESCO)./ Picha : Ikulu Tanzania 

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dunia kutumia Kiswahili katika kukuza utangamano na amani miongoni mwa wananchi wao.

Rais Samia alisema kuwa ni wazi lugh ahiyo ina nafasi kubwa katika kuwaleta watu pamoja na kufundisha maadili yaliyo mema.

''Natoa rai kwa viongozi wenzangu kote ulimwenguni kukitumia Kiswahili katika kukuza utangamano, kujenga na kulinda amani na mshikamano,'' alisema Rais Samia katika hotuba yake kwa taifa. ''Kiswahili ni fursa ya kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi zetu, bara letu la Afrika na duni akwa ujumla,'' Aliongeza Rais Samia.

Huu ni mwaka wa tatu wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani baada ya shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni ya Umoja wa Mataifa (UNESCO).

Katika kikao hicho mwaka 2021, UNESCO ilitambua jukumu la lugha ya Kiswahili katika kukuza tofauti za kitamaduni, kujenga ufahamu na kukuza mazungumzo kati ya ustaarabu na kubainisha haja ya kukuza lugha nyingi.

''Kiswahili ni lugha muhimu katika mawasiliano ya usawa kati ya watu, ambayo inakuza umoja katika utofauti na uelewa wa kimataifa, uvumilivu na mazungumzo,'' ilisema sehemu ya taarifa ya UNESCO.

Lugha ya ukombozi

Katika hotuba yake Rais Samia alipongeza juhudi zilizofanywa na wadau mbali mbali ndani na nje ya Tanzania katika kufundisha, kukikuza na kukieneza lugha hiyo.

Alisifia lugha ya Kiswahili kama chombo kilicho na umuhimu katika historia ya Tanzania na Afrika Mashariki hasa wakati wa kupigania uhuru.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Kiswahili, Elimu na Utamaduni wa Amani'.

Mama Samia amesema kuwa Kauli mbiu hii inaakisi historia na umuhimu wa siku iliyotengwa ya maadhimisho haya.

''Miaka 70 iliyopita, chama cha Ukombozi cha Tanganyika African National Union TANU, kiliazimia kwamba Kiswahili kitumike kama lugha rasmi ya kuwaunganisha watu katik aharakati za kudai uhuru wa Tanganyika,'' alisema Rais Samia katika hotuba yake.

Kiswahili kilitumika pia katika harakati za ukombozi wa Zanzibar, Kenya na nchi nyingine za Afrika

Rais Samia Suluhu Hassan

Kiswahili ni mojawapo ya lugha zinazotumiwa sana katika familia ya Kiafrika, na inayozungumzwa zaidi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 230.

TRT Afrika