Akitoa risala yake katika mkutano wa saba wa Mkuu wa Majeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Makamanda kwa mwaka 2023, Rais Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi hilo kujiandaa kikamilifu na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.
Rais Samia, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa nchi hiyo, amesisitiza umuhimu wa JWTZ, kwenye kamandi zake tofauti kujipanga na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu, na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2025.
"Tuko wengi, ni chaguzi zinazoshirikisha vyama vingi, vyenye nia tofauti...hatuoni kama kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa, kwa hiyo ni vyema mkajiweka tayari kwa chochote kile kitakachojitokeza," alisema Rais huyo wa Tanzania.
Hata hivyo, Rais Samia alitupilia mbali uwezekano wa matumizi ya nguvu kwa kulishirikisha jeshi kwenye michakato hiyo miwili, akisisitiza taratibu, sheria na miongozo ya chaguzi kufuatwa.
Alisema: Lakini ni vyema jeshi na vikosi vyote vya ulinzi na usalama kuwa tayari kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza.
Wakati huo huo, Tanzania imepokea waomba hifadhi zaidi ya 100,000 kutoka nchi tofauti, ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza katika mkutano huo wa maafisi waandamizi wa jeshi Tanzania, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda amesema Tanzania imepokea jumla ya waomba hifadhi 138,149 kati ya Januari 1, 2023 na Disemba 31, 2023.
Amesema, idadi kubwa ya waomba hifadhi hao wanatokea nchi za Rwanda, Burundi na DRC na wanaingia Tanzania kutafuta fursa za kiuchumi.