Rais wa senegal Macky Sall ametangaza kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Februari 25, hadi muda usiojulikana saa chache tu kabla ya kampeni rasmi kuanza.
Sall amebatilisha amri yake ya awali ya Novemba 2023 aliyosaini na kuweka uchaguzi kuwa Februari 25, huku wagombea 20 wakiwania ingawa wagombea wawili wakuu wa upinzani waliondolewa.
Wawili hao ni Ousmane sonko, ambaye amefungwa jela tangu Julai 2023, na Karim Wade, mwana wa rais wa zamani Abdoulaye Wade.
Rais Sall ametaja tofauti juu ya kutostahiki kwa baadhi ya wagombea na madai ya ufisadi katika kesi zinazohusiana na uchaguzi.
Kwenye hotuba yake kwa taifa Jumamosi, Sall alisema amesaini amri ya kufuta hatua ya awali iliyoweka tarehe hiyo, kwa sababu wabunge walikuwa wakichunguza majaji wawili wa Baraza la Katiba ambao uadilifu wao katika mchakato wa uchaguzi umetiliwa shaka.
"Nitaanza mjadala wazi wa kitaifa ili kuleta pamoja masharti ya uchaguzi huru, uwazi na umoja," Sall aliongeza, bila kutoa tarehe mpya.
Hii ni mara ya kwanza kwa uchaguzi wa Urais nchini humo kuahirishwa na linakuja kufuatia mzozo kati ya Bunge la Taifa na Mahakama ya Katiba juu ya kufungiwa kwa wagombea.
Licha ya rais huyo kusisitiza kwamba atampa mamlaka mapema mwezi Aprili kwa mshindi wa kura, baada ya kutangaza kwamba hatawania kwa muhula wa tatu, Sall alimteua Waziri mkuu Amadou Ba kutoka chama chake kuwa mrithi wake.
Wakati huo huo, Rose Wardini, mmoja wa wagombe wawili pekee wa kike kwenye orodha iliyoidhinishwa ya wagombea, alikamatwa Ijumaa kwa mashtaka ya madai ya kuficha uraia wake wa Ufaransa, kulingana na vyanzo vya mahakama.