Rais William Ruto wa Kenya ameonya kwamba mashambulizi dhidi ya maafisa wa mahakama nchini "hayapaswi kutokea tena" kufuatia kupigwa risasi kwa hakimu wa mahakama siku ya Alhamisi.
Rais Ruto, katika ujumbe wa rambirambi Jumatatu, alielezea tukio hilo kama "la kusikitisha" na "lisilokubalika."
"Najiunga na familia, marafiki, na jumuiya ya mahakama katika kuomboleza kifo cha kusikitisha cha Mheshimiwa Monica Kivuti, ambaye alikuwa akihudumu kama Hakimu Mkuu wa Mahakama za Makadara,'' Rais Ruto aliandika kwenye akaunti yake ya X Jumatatu.
Monica Kivuti alipigwa risasi Alhamisi baada ya kukataa ombi la dhamana la mke wa afisa wa polisi. Mshambuliaji, ambaye hakutajwa jina, alipigwa risasi na kuuawa na maafisa wengine wa polisi.
Jumamosi, jaji mkuu wa nchi hiyo, Martha Koome, alitangaza kwamba Kivuti alifariki kutokana na majeraha yake.
"Katika hali yoyote ile, hawapaswi (polisi) kuacha jukumu hili muhimu au kugeuka kutoka kwa wajibu wao wa ulinzi na kuwa tishio kwa usalama na usalama wa watu. Kilichotokea kwa Mheshimiwa Kivuti hakikubaliki; hakipaswi kutokea tena,” Ruto alionya.
Maafisa wengine watatu walijeruhiwa baada ya tukio la kupigwa risasi.
Jaji Mkuu Martha Koome aliagiza kwamba bendera zote za Mahakama zipunguzwe nusu mlingoti kwa heshima ya Hakimu Kivuti.
“Familia ya mahakama inasimama kwa mshikamano wakati huu wa huzuni kubwa na inatoa wito wa kuonyesha hisia na huruma tunaposhiriki katika maombolezo,” Koome alisema katika tangazo.
"Nawaomba polisi kuhakikisha usalama wa maafisa wetu wa mahakama wakati wote wanapotekeleza majukumu yao. Tumepoteza mtaalamu thabiti na mchapakazi wa mahakama ambaye aliwahudumia Wakenya kwa kujitolea,” alisema Rais Ruto.