Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amemkaimisha madaraka Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Angie Motshekga, baada ya kiongozi huyo kuwa anahudhuria mkutano wa kanda ya SADC unaofanyika nchini Zimbabwe, ofisi ya Rais ya nchi hiyo imesema katika mtandao wake, siku ya Jumamosi.
Ramaphosa tuko jijini Harare, akihudhuria Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kulingana na katiba ya Afrika Kusini, kiongozi mwandamizi katika serikali atakaimishwa madaraka ya urais wakati Rais yuko nje ya nchi.
Hii ni mara ya pili kwa Motshekga kukaimu nafasi hiyo ya juu nchini humo, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 2021 wakati Rais Ramaphosa alipohudhuria mazishi ya Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda.
Hatua ya Rais Ramaphosa inakuja baada ya kuchaguliwa kwa serikali ya kwanza ya mseto nchini humo tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi mwaka 1994.
Serikali ya Mseto
Chama cha ANC, ambacho kimekuwa kikiongoza Afrika Kusini tangu kuangushwa kwa utawala wa kibaguzi, kilipoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Mei, na kukilazimisha kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na vyama vingine vya siasa.
Hali ya kisiasa katika moja ya mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika imesalia kuwa ya wasiwasi tangu uchaguzi, huku ushindani kati ya Rais wa zamani Jacob Zuma na Ramaphosa ukiendelea.
Ajenda za mkutano
Wakuu wa nchi za SADC wanakutana jijini Harare kwa mkutano wa 44 wa kanda hiyo.
Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu "Kukuza ubunifu ili kufungua fursa za ukuaji endelevu wa uchumi na maendeleo kuelekea SADC ya viwanda."
Mkutano huo utashuhudia Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe akichukua nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya hiyo yenye wanachama 16, akichukua nafasi ya Rais wa Angola Joao Lourenco.