Rais wa Rwanda Paul Kagame amewalaumu viongozi wa kidini kwa kuwalaghai na kuwapotosha waumini wao katika mahubiri.
Rais Kagame alilalamika kuwa viongozi hao wamesahau majukumu yao ya kufuata mitindo ya maisha yanayotoa mfano wa kuigwa na waumini.
''Je, Mungu anakuambia anapokutokea kwamba uende kuua watu au kusema uwongo au hata kuwaibia? Ikiwa ni kweli kwamba anaonekana kwako, ningefurahi kusikia ujumbe aliokupa,'' alisema Rais Kagame.
Rais Kagame alikuwa akihutubia viongozi wa kisiasa, viongozi wa kidini pamoja na wageni wengine wakati wa dhifa ya Kifungua kinywa ya Maombi ya Shukrani kilichoandaliwa na Rwanda Leaders Fellowship (RLF) kutoa shukrani kwa Mungu kwa uchaguzi uliofanikiwa na wa amani.
Akizungumzia juu ya hatua ya kufunga makanisa nchini Rwanda, hasa yale ambayo hayakidhi mahitaji, Kagame alisema kwamba serikali haiwezi kukaa kimya wakati makanisa mengi yaliyokuwa yakiibuka yalikuwa yanapotosha watu na wakati huo huo kuwanyang'anya rasilimali zao walizochuma kwa bidii.
''Ukijifanya Mungu amekutokea ukaanza kuwapotosha watu ukiwaambia wakatae kula, wakatae matibabu, umetumwa na nani? Si Mungu pekee bali hata mwanadamu mwenye akili timamu hawezi kukutuma kufanya mambo kama hayo. Na unatudanganya kuwa umetumwa na Mungu?'' aliuliza Rais Kagame.
Rais Kagame alisema alitoa onyo kwa wale wanaojaribu kumshutumu kuwa anashambulia makanisa akisema kuwa hawawezi kutishwa katika kutekeleza haki.
Pia Rais Kagame aliwataka waumini wasiwe na woga wa kumkosoa kiongozi yeyote wa kidini wanaposhuhudia akifanya mambo ya kinafiki.
Zaidi ya makanisa 4,000 yalifungwa mnamo mwezi Agosti nchini Rwanda kwa kushindwa kufuata kanuni za afya na usalama, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na vidhibiti sauti.