Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametuma rambirambi kwa raia na serikali ya Morocco kufuatia tetemeko la ardhi Morocco lililosababisha vifo vya watu 632 huku shughuli ya uokoaji ikiendelea.
Tetemeko hilo la ukubwa wa 7.0 liligonga takriban kilomita 72 Kusini Magharibi mwa eneo la watalii la Marrakech saa 11:11 (tano) usiku , Utafiti wa Jiolojia wa Marekani uliripoti.
"Rafiki na nchi ndugu, natuma salamu zangu za heri kwa watu wote wa Morocco walioathiriwa na maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea Morocco." Rais Erdogan alisema.
Rais wa Uturuki Erdogan ambaye yuko New Delhi kuhudhuria Mkutano wa G20 nchini India, aliwaongoza viongozi mbalimbali wa dunia katika kuomboleza na raia wa Morocco kufuatia tetemeko hilo.
"Nawatakia rehema za Mwenyezi Mungu kwa wale waliopoteza maisha na nawatakaia uponyaji wa haraka waliojeruhiwa. Tunasimama karibu na kaka na dada zetu wa Morocco kwa uwezo wetu wote katika siku hii ngumu." Rais Erdogan alimaliza.
Aidha, Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki nayo imesema kuwa Uturuki itasimama na Morocco katika kipindi hiki kigumu.
Tetemeko hilo la ardhi pia lilisikika katika nchi jirani ya Algeria, ambapo Ulinzi wa Raia wa Algeria ulisema haukusababisha uharibifu wowote au majeruhi.