Raia 20 wauawa katika shambulio la silaha huko Darfur, Sudan

Raia 20 wauawa katika shambulio la silaha huko Darfur, Sudan

Watu wenye silaha waliwafyatulia risasi raia katika jimbo la Darfur Kaskazini
Takriban raia 863 wameuawa na maelfu kujeruhiwa katika mapigano kati ya mahasimu hao wawili wa kijeshi tangu Aprili. Picha AA

Takriban raia 20 waliuawa katika shambulio la silaha katika jimbo la Darfur Kaskazini magharibi mwa Sudan, kwa mujibu wa gavana wake.

Nimir Abdulrahman aliiambia Anadolu kwamba watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki na magari ya SUV waliwafyatulia risasi wakaazi katika mji wa Kutum, magharibi mwa mji mkuu wa jimbo la Al-Fasher Jumapili jioni.

Hakutoa maelezo zaidi kuhusu shambulio hilo, akitaja kutatizika kwa huduma za mawasiliano katika eneo hilo.

Hata hivyo gavana huyo hakupuuza kuwa shambulio hilo linahusishwa na mapigano yanayo endelea nchini Sudan kati ya jeshi na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF).

Takriban raia 863 wameuawa na maelfu kujeruhiwa katika mapigano kati ya mahasimu hao wawili wa kijeshi tangu Aprili 15, kulingana na matabibu wa eneo hilo.

AA