Polisi wa Sudan Kusini walisema katika taarifa mnamo Januari 20, 2025: "Raia kumi na sita wa Sudan waliripotiwa kuuawa katika majimbo manne." / Picha: Reuters

Polisi wa Sudan Kusini walisema siku ya Jumatatu kuwa raia 16 wa Sudan waliuawa katika ghasia wiki iliyopita kutokana na madai ya mauaji ya watu wa Sudan Kusini katika eneo la Al Jazirah nchini Sudan.

Ghasia zilizuka katika mji mkuu wa Sudan Kusini Juba na kwingineko nchini humo siku ya Alhamisi na Ijumaa, huku waandamanaji wakiwa na hasira kwa kile walichoamini kuwa ni kuhusika kwa wanajeshi wa Sudan na makundi washirika katika mauaji ya Al Jazirah.

Jeshi la Sudan limelaani kile lilichokiita "ukiukwaji wa watu binafsi" huko Al Jazira baada ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kulilaumu na washirika wake kwa mashambulizi yaliyolengwa kikabila dhidi ya raia wanaotuhumiwa kuunga mkono Vikosi vya waasi vya RSF .

Polisi nchini Sudan Kusini ilisema katika taarifa: "Raia kumi na sita wa kigeni wa Sudan waliripotiwa kuuawa katika majimbo manne."

Amri ya kutotoka nje jioni hadi alfajiri

Polisi wataendelea kushika doria katika masoko na maeneo ya makazi ili kuwalinda watu wa Sudan, ilisema taarifa hiyo.

Siku ya Ijumaa, serikali iliweka amri ya kutotoka nje kuanzia jioni hadi alfajiri, ambayo bado inatumika.

Takriban washukiwa 24 wamekamatwa na mashtaka yatawasilishwa mara tu uchunguzi utakapokamilika, jeshi la Sudan Kusini lilisema katika taarifa tofauti.

TRT Afrika