Huduma imesambaratika katika hospitali za Port Sudan huku Umoja wa mataifa ukisema kuwa magonjwa kama  malaria, surua na homa ya dengue, yanaongezeka. / Picha : Reuters 

Masaibu ya Sudan yameendelea kuchukua mkondo mpya katika mji wa pwani wa Port Sudan, huku hali ya afya ikisemekana kuzorota kutokana na tangazo la mgomo wa madaktari.

Mji huo unaodhibitiwa na jeshi umekuwa kimbilio kutoka kwa vita vinavyoendelea magharibi mwa nchi, lakini mfumo wake wa afya unakaribia kuporomoka kutokana na kukatika kwa umeme na uhaba wa vifaa - na uhaba wa wafanyakazi sasa umechangiwa na madaktari wanaogoma.

Vita kati ya jeshi la taifa na kikosi cha dharura RSF vimeendelea kwa zaidi ya miezi mitano sasa na vimehujumu shughuli nyingine za serikali.

"Inachosha, kuna wagonjwa wengi na kuna mateso mengi," Omar al-Saeed, muuguzi anayegoma katika hospitali ya kufundisha ya Port Sudan, ameambia shirika la Reuters.

"Tunadai tu walipe watu kitu kidogo ili waendelee." Aliongeza.

Madaktari na wauguzi katika mji wa Bahari Nyekundu wanasema hawajalipwa mishahara kwa miezi minne.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya 100,000 wamekimbilia mji huo wa Port Sudan, wakijaza hospitali na makazi ya jiji hilo lenye watu wengi, huku mapigano yakilenga Khartoum na magharibi mwa nchi hiyo.

Mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths ameonya kwamba vita hivyo vinachochea "dharura ya kibinadamu ya kiwango kikubwa" na kwamba magonjwa kadhaa, ikiwa ni pamoja na malaria, surua na homa ya dengue, yanaongezeka.

TRT Afrika