Polisi katika jiji la biashara nchini India wamefungua kesi ya uhalifu dhidi ya mmiliki wa bango kubwa la biashara ambalo limeanguka katika kituo cha mafuta na kusababisha vifo vya watu 14, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo.
Bango lenye ukubwa wa mita 70 kwa 50 mashariki mwa Mumbai limeanguka siku ya Jumatatu kutokana na upepo mkali ulioambatana na mvua kali.
Mamlaka ya eneo hilo imethibiisha Jumanne kufariki kwa watu 14 katika ajali hiyo, huku zaidi ya 75 wakijeruhiwa, wakati shughuli ya uokoaji ikiendelea.
"Matibabu hivi sasa yanaendelea kutolewa kwa watu 44 waliojeruhiwa, 31 tayari wameruhusiwa baada ya kupata matibabu," imesema manispaa ya mji kupitia mtandao wa kijamii wa X.
"Kwa bahati mbaya, watu14 wamepoteza maisha katika ajali hiyo," imeongeza. "Shughuli za uokoaji zinaendelea katika eneo la ajali."
Gaurav Chauhan kutoka kikosi cha taifa cha kukabiliana na majanga (NDRF) ameiambia AFP kwamba bango lililoanguka katika kituo cha mafuta limefanya shughuli ya uokoaji kuwa mgumu.
"Tumeshindwa kutumia vifaa kwa sababu ya kuhofia moto na majanga mengine, kwa hivyo tunatumia matingatinga kuondoa vifusi," amesema.