Polisi wa Kenya watua Haiti huku Waziri mkuu akiapa kutwaa tena udhibiti wa nchi

Polisi wa Kenya watua Haiti huku Waziri mkuu akiapa kutwaa tena udhibiti wa nchi

Misheni hii imekumbwa na ati ati tangu mwanzo huku baadhi wakihoji uwezo wa polisi wa Kenya kudhibiti magenge hayo.
Vita vya magenge hivi sasa vimewakosesha makazi zaidi ya watu nusu milioni na karibu milioni tano wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula./ Picha: Reuters 

Kikosi cha kwanza cha polisi wa Kenya kiliwasili katika mji mkuu wa Haiti siku ya Jumanne kuanza misheni iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu ya kulinda amani katika nchi ya Caribbean ambayo imekumbwa na ghasia za magenge, huku kukiwa na shaka kutokana na maandamano waliyoacha nyumbani.

"Hatimaye jeshi la kimataifa liko hapa kusaidia polisi wetu wa kitaifa," Waziri Mkuu wa Haiti Garry Conille alisema katika mkutano na waandishi wa habari, akisema kazi ya kuchukua tena nchi itaanza "polepole, bila mapigano makubwa isipokuwa lazima."

"Lakini sitaki mtu yeyote atilie shaka malengo yetu," alisema. "Jimbo litapata tena mamlaka na kuthibitisha mamlaka yake ili Wahaiti wote waishi kwa amani katika nchi hii."

Misheni hiyo iliombwa kwa mara ya kwanza na serikali ya awali ya Haiti mwaka wa 2022. Lakini uungwaji mkono ulidorora na mtangulizi wa Conille alilazimika kujiuzulu mapema Machi baada ya kusafiri hadi Nairobi kupata uungwaji mkono wa Kenya huku ghasia zikiongezeka huko Haiti.

Vita vya magenge hivi sasa vimewakosesha makazi zaidi ya watu nusu milioni na karibu milioni tano wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Makundi yenye silaha, ambayo sasa yanadhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu, yameunda muungano mpana huku yakitekeleza mauaji yaliyoenea, utekaji nyara na unyanyasaji wa kingono.

"Madhumuni ya pekee ya Kenya ni kutumika kama mawakala wa amani," Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Monica Juma aliuambia mkutano na waandishi wa habari, akisema polisi watatoa kipaumbele kwa kulinda raia, kufungua njia za usafirishaji wa watu, bidhaa na misaada ya kibinadamu, na kulinda taasisi za serikali.

wingu la shaka

Misheni hii imekumbwa na ati ati tangu mwanzo huku baadhi wakihoji uwezo wa polisi wa Kenya kudhibiti magenge hayo.

Pia kumetokea madai yasiyothibitishwa kuhusu malipo ya polisi hao ambao baadhi wanadaiwa kutopokea pesa kamili walizoahidiwa kabla ya kuanza safari yao.

Lakini hata polisi wa Kenya waliovalia sare waliposhuka kutoka kwa ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways wakiwa na silaha mkononi katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince, wenzao huko Nairobi walikuwa na changamoto kubwa kukabiliana na vijana wa Gen Z waliowashinda nguvu nakupeleka maandamano yao hadi majengo ya bunge.

Polisi hao walishutumiwa pia kutumia nguvu kupita kiasi huku zaidi ya watu watano wakifariki kutokana na majeraha ya risasi, jambo ambalo limeshutumiwa vikali na makundi ya haki za binadamu.

Katika hotuba ya dharura kwa taifa usiku wa Jumanne, Rais William Ruto aliahidi uchunguzi utafanywa juu ya ukiukaji wowote wa haki za waandamanaji huku akisisitiza kuwa, japo kuna uhuru wa kuandamana, polisi pia wana jukumu la kujilinda, na kulinda mali na amani ya wananchi.

TRT Afrika na mashirika ya habari