Ongezeko la nishati hiyo linatokana na kupanda kwa gharama za mafuta yaliyosafishwa katika soko la Kimataifa./Picha: Wengine  

Watumiaji wa nishati ya petroli katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam, sasa watalazimika kulipia 3,163 kwa lita moja Petroli, Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji ya Tanzania(EWURA), imesema.

Ongezeko hilo linafuatia kupanda kwa asilimia 4.5 kwa gharama ya Petroli katika soko la Kimataifa.

Mabadiliko katika soko la kimataifa, pia yameathiri bei ya Dizeli na Mafuta ya Taa kwa rejareja, ambazo kwa sasa yatakuwa yanapatikana kwa 3,146 na 2,840 mtawalia.

"Mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Machi 2024 yamechangiwa na ongezeko la bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 4.5 kwa mafuta ya petroli na asilimia 1.99," imesomeka sehemu ya taarifa ya mdibiti huyo.

Kulingana na EWURA, mabadiliko hayo pia yamechangiwa pia na ongezeko la matumizi ya sarafu ya Euro katika kulipia mafuta yaliyoagizwa.

Kwa upande wa mji wa Arusha, ambao ni kitovu cha utalii wa Tanzania, mafuta ya Petroli yananuliwa kwa 3,247 kwa lita, wakati Dizeli inauzwa kwa 3,211 na Mafuta ya Taa yatanunuliwa 2,924 kwa lita ya bei ya rejareja katika vituo vya mafuta.

Mamlaka hiyo, pia imevitaka vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

Ikumbukwe pia, kwa mwezi wa Februari 2024, mafuta ya Petroli yalikuwa yakinunulika kwa 3,051 kwa lita, Dizeli ikiuzwa kwa 3,029 wakati Mafuta ya Taa yalinunulika kwa 2,924 kwa lita.

TRT Afrika