Mapigano kati ya makundi ya kijeshi sasa yapo katika wiki yake ya nane na yamewaathiri raia | Picha: AA

Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka vya kijeshi vinatarajiwa kuanza tena mazungumzo yanayo ungwa mkono na Marekani na Saudi Arabia, kulingana na ripoti.

Shirika la habari la Reuters, likinukuu Televisheni ya Al Arabiya, lilisema pande hizo mbili zimekubaliana kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja bila kutoa maelezo zaidi.

Jeshi na RSF hawajatoa maoni yao kuhusu maendeleo haya ya hivi punde.

Mapigano kati ya makundi ya kijeshi sasa yapo katika wiki yake ya nane na yamewaathiri raia, hivyo kuwakatisha fursa ya kupata huduma za kimsingi.

Makubaliano ya wiki moja ya kusitisha mapigano yaliyo kubaliwa mwishoni mwa mwezi Mei yaliathiriwa na mashambulizi ya anga, milio ya risasi na milipuko saa chache baada ya majenerali wapinzani kufanya mapatano hayo.

Kiongozi wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, anasema amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Faisal bin Farhan, ambapo alisisitiza haja ya RSF kuondoka katika hospitali, vituo vya umma, na nyumba.

Kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo alisema Jumapili alikuwa amezungumza na Farhan na kuelezea kuunga mkono kwake kufungua korido za kibinadamu. Hakuna kiongozi hata hivyo aliyetaja mazungumzo ya kuanza upya.

Zaidi ya raia 400,000 wamekimbia kuvuka mipaka ya Sudan na zaidi ya milioni 1.2 kutoka Khartoum na miji mingine.

TRT Afrika