Ujerumani imemfukuza balozi wa Chad mjini Berlin katika hatua ya kujibu mapigo huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kati ya nchi hizo mbili.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani iliikosoa serikali ya mpito ya kijeshi ya Chad kwa kumtangaza balozi wa Ujerumani "persona non grata" wikendi iliyopita.
Sasa imelipiza kisasi kwa kumfukuza mjumbe wa Chad, Mariam Ali Moussa.
“Katika kukabiliana na kufukuzwa bila msingi kwa balozi wetu nchini Chad, leo tumemwita balozi wa Chad mjini Berlin, Mariam Ali Moussa, na kumtaka aondoke Ujerumani ndani ya saa 48. Tunasikitika kwamba ilibidi kufikia hili,” wizara hiyo ilisema kwenye Twitter.
Pia ilisema Balozi wa Ujerumani Gordon Kricke, ambaye alifukuzwa kutoka Chad wiki iliyopita, alitekeleza majukumu yake "kwa njia ya kupigiwa mfano," na alifanyia kazi haki za binadamu na mpito wa haraka hadi serikali ya kiraia katika nchi hiyo ya Afrika ya kati.
Ilisema kwamba ubalozi wa Ujerumani nchini Chad ungeendeleza kazi hii “pamoja na washirika wetu mashinani.” Ujerumani bado ina wanadiplomasia wa ngazi za chini mjini N'Djamena.
Wizara ya Mawasiliano ya Chad ilisema wiki iliyopita kwamba mwanadiplomasia mkuu wa Ujerumani nchini humo alitangazwa kuwa "persona non grata" kutokana na "mtazamo wake wa utovu wa adabu na kutoheshimu desturi za kidiplomasia."
Ripoti za vyombo vya habari zimeashiria ukosoaji wa serikali ya mpito ya Chad kama sababu inayowezekana ya kufukuzwa kwa balozi wa Ujerumani.
Baada ya kifo cha rais wa muda mrefu wa Chad Idriss Deby Itno mwaka 2021, jeshi lilimtaja mtoto wake wa kiume, Mahamat Idriss Deby, kuwa kiongozi wa muda wa nchi hiyo kwa kipindi kilichokusudiwa kuwa cha miezi 18.
Hata hivyo, mwaka jana serikali ilitangaza kuongeza muda wa mpito kwa miaka miwili zaidi, jambo ambalo lilisababisha maandamano kote nchini.