Nigeria: Umeme wakatika, viwanja vya ndege vyafungwa vyama vya wafanyakazi vikigoma

Nigeria: Umeme wakatika, viwanja vya ndege vyafungwa vyama vya wafanyakazi vikigoma

Mgomo ulianza kufuatia kuvunjika kwa mazungumzo kati ya serikali na vyama vikubwa vya wafanyakazi nchini humo.
Mgomo huo wa Juni 3, 2024 umesababisha shughuli nyingi kusimama./Picha: Reuters

Mgomo wa vyama vya wafanyakazi nchini Nigeria umeingia siku yake ya pili Jumanne, huku sekta kadhaa muhimu zikiwemo za usafiri, elimu, benki na huduma za afya zikiathiriwa kwa kiasi kikubwa.

Vyama vya wafanyakazi nchini humo wanataka ongezeko la kima cha chini cha mshahara kutoka dola 20 mpaka 67.

Serikali ya nchi hiyo imependekeza kuongeza kima cha chini mara mbili kufikia walau dola 40, kufuatia kikao na vyama hivyo siku ya Jumatatu.

Pande zote mbili zimepanga kuendelea kukutana wiki hii kufanikisha azma ya kuondoa migomo hiyo.

Wengi waathirika

"Hakuna mfanyakazi ambaye angedhulumiwa kutokana na mgomo huu," taarifa iliyotiwa saini na pande zote mbili, akiwemo Waziri wa Kazi wa Nigeria Nkeiruka Onyejeocha na maafisa wa chama cha wafanyakazi, ilisema.

Vyama vya wafanyakazi nchini Nigeria ina mamilioni ya wanachama wanaotoa huduma muhimu kwenye sekta mbalimbali.

Mgomo huo uliathiri abiria wengi kwenye viwanja vya ndege siku ya Jumatatu kufuatia mgomo huo. Vyama hivyo vimesema kuwa hakutakuwa na safari za ndege za kimataifa siku ya Jumanne.

Gazeti la Punch la nchini Nigeria limeripoti kuwa wafanyakazi hao "walifunga milango ya kuingilia uwanja wa ndege wa Lagos."

Vyama vya wafanyakazi kuendeleza mgomo

Wafanyakazi wa uwanja wa ndege walilazimika kuwajulisha abiria juu ya kukosekana kwa safari za ndege hadi kumalizika kwa mgomo huo.

Mgomo huo pia uliathiri kwa kiasi kikubwa sekat ya afya huku huduma za dharura tu, zikitolewa katika mji wa Abuja.

Huduma zingine zilizoathiriwa na mgomo huo ni pamoja na taasisi za fedha, shule, bandari na ofisi za serikali.

Hata hivyo vyama hivyo vimeazimia kuendelea na mgomo.

TRT Afrika