Wanigeria hutumia takriban tani milioni 12 za mahindi kwa mwaka. / Picha: Reuters

Baraza la Seneti la Nigeria limepitisha mswada unaotaka kuifanya kuwa kosa la jinai kuuza nje kiasi kikubwa cha mahindi ambayo hayajasindikwa katika juhudi za kupunguza njaa katika taifa hilo la Afrika Magharibi, stakabadhi zilizoonekana na Reuters siku ya Ijumaa zilionyesha.

Nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika inapambana na mzozo mbaya zaidi wa gharama ya maisha kuwahi kutokea katika kizazi.

Matatizo ya kiuchumi yamekuwa mabaya zaidi tangu Rais Bola Tinubu aanze mageuzi ya kubana matumizi, ikiwa ni pamoja na kushusha thamani ya sarafu ya nchi hiyo naira na kukomesha ruzuku ya petroli iliyodumu kwa miongo kadhaa, na hivyo kuchochea mfumuko wa bei.

Sarafu dhaifu ya Nigeria imechochea mauzo yasiyo rasmi ya Mahindi, mchele na mtama kwa nchi jirani kutokana na tofauti ya kiwango cha ubadilishaji na faranga ya CFA ya Afrika Magharibi.

Chakula kikuu

Mahindi ni chakula kikuu nchini Nigeria ambacho pia hutumika kwa chakula cha mifugo, vinywaji na unga uliosindikwa.

Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA) inatabiri kupanda kwa mauzo ya mahindi ya Nigeria 2024/25 hadi tani 75,000 kutoka kwa makadirio yake ya 2023/24 ya tani 50,000.

Mswada wa Seneti, ambao utahitaji kibali cha rais ili kuwa sheria, utafanya kuwa kinyume cha sheria kusafirisha mahindi ambayo hayajasindikwa kutoka kwa kiwango cha chini cha tani 1 ya metriki.

Wakiukaji wangelipa thamani ya mahindi kwa faini au watakabiliwa na kifungo cha mwaka mmoja jela.

Ukosefu wa chakula

Ripoti ya pamoja ya serikali ya Nigeria na Umoja wa Mataifa ilisema mwezi Novemba kuwa zaidi ya watu milioni 30 wanatarajiwa kuwa na uhaba wa chakula mwaka ujao, ikiwa ni ongezeko la theluthi moja kutoka mwaka huu.

USDA inakadiria kuwa Nigeria hutumia takriban tani milioni 12 za mahindi kwa mwaka, ikiagiza kutoka nje takriban tani 100,000.

TRT Afrika