Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametaka kiongozi wa Niger Mohamed Bazoum aachiliwe huru na kuongeza wasiwasi wake mkubwa juu ya kile alichokiita hali ya kusikitisha ya kuzuiliwa kwa kiongozi wa Niger Mohamed Bazoum.
Kulingana na taarifa ya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu Antonio Guterres Jumatano alishutumu "hali mbaya ya maisha ambayo Rais Bazoum na familia yake wanaripotiwa kuishi".
CNN iliripoti kuwa Bazoum anazuiliwa kwa kutengwa na kulazimishwa kula wali kavu na tambi na waasi waliompindua katika mapinduzi mwishoni mwa mwezi uliopita.
Katika msururu wa ujumbe mfupi wa simu uliotumwa na Bazoum kwa rafiki yake, rais alisema "amenyimwa mawasiliano na mwanadamu tangu Ijumaa", na hakuna mtu anayempa chakula au dawa, shirikia hilo liliripoti.
Guterres anasisitiza wasiwasi wake juu ya afya na usalama wa Rais na familia yake na kwa mara nyingine anatoa "wito wa kuachiliwa mara moja, bila masharti na kurejeshwa kama Mkuu wa Nchi," msemaji wa mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema katika taarifa.
Hali 'katili', 'isiyo ya kibinadamu'
Bazoum aliondolewa madarakani Julai 26 katika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Abdourahmane Tchiani, kamanda wa zamani wa walinzi wa rais wa Niger, ambaye amejitangaza kuwa mkuu wa serikali ya mpito.
Tangu wakati huo, Bazoum ameripotiwa kushikiliwa mateka katika ikulu ya rais katika mji mkuu Niamey. Yeye na familia yake wanazuiliwa chini ya hali ya "katili" na "isiyo ya kibinadamu" bila kupata maji ya bomba, umeme, bidhaa safi au madaktari, Chama chake cha Niger kwa Demokrasia na Ujamaa-Tarayya kilisema katika taarifa.
Junta haikutoa maoni mara moja juu ya hali ya maisha ya Bazoum.
Lakini kikikemea hali ya maisha, chama hicho kimetaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati ili kupata uhuru wake kutoka kwa kifungo cha nyumbani na kurejesha utulivu wa kikatiba. Junta imeapa kwamba haitakubali shinikizo la kuachia madaraka kama inavyotakiwa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).