Niger: Junta yamfukuza balozi wa Ufaransa

Niger: Junta yamfukuza balozi wa Ufaransa

Balozi wa Ufaransa amepewa saa 48 kuondoka nchini humo.
Jenerali Abdourahmane Tchiani alijitangaza kuwa kiongozi mpya wa Niger baada ya mapinduzi. PICHA / REUTERS

Watawala wa kijeshi ambao walichukua udhibiti huko Niamey mnamo Julai 26 wamempa balozi wa Ufaransa masaa 48 kuondoka Niger, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo alisema katika taarifa yake Ijumaa.

Kufuatiua "kukataa kwa balozi wa Ufaransa huko Niamey kujibu mwaliko" kutoka kwa waziri wa mkutano wa Ijumaa na "hatua zingine za serikali ya Ufaransa kinyume na masilahi ya Niger", viongozi wameamua kuondoa idhini yao kwa Sylvain Itte na kumwomba aondoke ndani ya saa 48, taarifa hiyo ilisema.

Uamuzi huu unafuatia mfululizo wa kauli na maandamano ya chuki dhidi ya Ufaransa tangu jeshi la Niger lilipompindua Rais Mohamed Bazoum, ambaye amezuiliwa na familia yake.

Viongozi hao wa kijeshi wanaishutumu Paris kwa kutaka kuingilia kijeshi nchini Niger ili kuirejesha Bazoum na kudai kuwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ni shirika lililo katika mfuko wa ukoloni wa zamani wa Ufaransa.

ECOWAS imeiwekea Niger vikwazo vizito vya kiuchumi kufuatia mapinduzi hayo na imetishia matumizi ya silaha kurejesha utulivu wa kikatiba.

Ufaransa ina takriban wanajeshi 1,500 walioko Niger kusaidia katika kupambana na makundi ya kijihadi ambayo yamekuwa yakiisumbua nchi hiyo pamoja na eneo kubwa la Sahel kwa miaka mingi.

TRT Afrika