Lynne Wachira
TRT Afrika, Nairobi, Kenya
Bingwa mara mbili wa michezo ya Olimpiki katika mbio za marathon, Eliud Kipchoge ametangaza rasmi kuwa atafungua msimu wa mwaka ujao mnamo mwezi Machi kwenye mbio za mji mkuu wa Tokyo, nchini Japan.
Huku michezo ya Olimpiki ikifanyika mwaka ujao mjini Paris, wengi wamekuwa wakisubiri kuona bingwa mtetezi wa Marathon angechagua mbio zipi kabla ya kujitosa ulingoni kutetea taji lake.
“Ninajivunia sana kupata nafasi kushiriki mashindano ya Tokyo, nilizichagua mbio hizi haswa kwa sababu zinafanyika mapema mwakani, ina maana kuwa nitapata muda wa kutosha kupumzika na kuanza maandalizi ya olimpiki huku mwaka ukiwa ungali mchanga.” Kipchoge aliiambia TRT Afrika Swahili kutoka kambi yake ya mazoezi nchini Kenya.
Kipchoge atakuwa anarejea mjini Tokyo kwa mara ya pili baada ya kushiriki na kutwaa ushindi katika Mbio za 2021 kwa kutumia muda wa 2:02:40.
Tokyo Marathon ni kati ya mashindano mengine ya miji mikuu kama vile London, New York, Boston, Chicago, na Berlin, yakiwa ndiyo mashindano ya ngazi ya juu zaidi katika mbio za Marathon.
“Mbio za Tokyo zina maandalizi ya hali ya juu sana lakini zaidi ya hayo nina kumbukumbu nyingi nzuri kutoka Tokyo na Japan kwa jumla, haswa ikizingatiwa kuwa mafanikio yangu yote ya mwaka wa 2021 niliyapata nchini humo, nilishinda mashindano ya mji wa Tokyo mwezi Machi na baadaye nikawa bingwa wa olimpiki mara mbili baada ya kushinda katika michezo ya Olimpiki ya Tokyo.”
“Inapendeza sana kufahamu kuwa nitapata nafasi ya kutangamana na mashabiki wa riadha kwani ilikuwa vingumu kwa waandalizi kushirikisha mashabiki kwa sababu za kanuni zilizowekwa kukabiliana na janga la Uviko -19 mwaka 2021.”
Iwapo Kipchoge atafanikiwa kutetea taji lake la Olimpiki, basi ataandika historia kama mwanariadha wa kwanza kabisa wa Marathon kutwaa ubingwa wa olimpiki mara tatu.
“Ndoto yangu ni kuibuka bingwa wa Olimpiki, itakuwa ni raha isiyo kifani kutimiza ndoto hii mjini Paris, ninafanya juhudi kuhakikisha kuwa maandalizi yangu yatakuwa ya kiwango cha juu.”
Kipchoge ni kati ya kikosi cha Olimpiki ambacho kilitajwa hivi majuzi na shirkisho la riadha nchini Kenya – kikosi hicho cha wanariadha kumi kitapunguzwa hadi wanariadha watatu ifikapo mwaka ujao.
Wengi watakuwa wanafuatilia kwa karibu mashindano ya Kipchoge mjini Tokyo haswa baada ya rekodi yake ya dunia kuvunjwa na Mkenya mwingine, Kelvin Kiptum katika mbio za mji mkuu wa Chicago mwezi Oktoba.
Mwaka huu Kipchoge alishiriki mbio za Boston Marathon mwezi Aprili ambapo alimaliza katika nafasi ya sita kabla ya kujinyanyua na kushiriki mbio za mji mkuu wa Berlin mwezi Septemba ambapo aliandikisha historia kama mwanariadha wa kwanza kushinda mbio za Berlin mara tano.