Shirika la Ndege la TUI la nchini Uholanzi, limejeresha safari zake katika Ukanda wa Afrika Mashariki, baada ya miaka ya sita./Picha: @KATAKenya   

Shirika la Ndege la TUI la nchini Uholanzi, limejeresha safari zake katika Ukanda wa Afrika Mashariki, baada ya kuzisitisha kwa kipindi cha miaka ya sita.

Novemba 5, 2024, ndege aina ya Boeing Dreamliner ilitua katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Moi jijini Mombasa nchini Kenya, kwa mara ya kwanza baada ya miaka sita kufuatia kudorora kwa hali ya usalama na mlipuko wa Uviko-19.

Kulingana na shirika hilo, kutakuwa na safari mbili kwa wiki kati ya jiji la Amsterdam na Mombasa, hatua ambayo inalenga kukuza utalii wa eneo hilo la pwani ya Kenya.

Pia inalenga kuwa na safari za idadi hiyo hiyo, katika visiwa vya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia iliyotolewa Julai 29, 2021, hali ya uchumi wa Zanzibar iliathirika zaidi ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na kushuka kwa mapato yatokanayo na utalii ambapo uwiano wa vyumba vinavyokaliwa katika hoteli visiwani humo, ulishuka.

Hali hii ilichangia kushuka kwa Pato la Taifa la Zanzibar mpaka asilimia 1.3. Hii ni tofauti na kipindi cha nyuma, hususan kati ya mwaka 2017 na 2019, ambapo ukuaji wa uchumi wa Zanzibar ulikua kwa wastani wa asilimia 7, kwa mujibu wa makisikio ya Wizara ya nchi, Afisi ya rais wa Zanzibar Fedha na Mipango.

TRT Afrika