Nchi nane katika ukanda wa pembe ya Afrika, ikiwemo na Rwanda, zinatarajiwa kushuhudia mvua zisizo za kawaida, Taasisi ya Ubashiri wa Hali ya Hewa (ICPAC) imesema siku ya Jumanne.
“Mvua zisizo za kawaida zitashuhudiwa katika maeneo mengi ya Uganda, Kenya, kaskazini mwa Burundi, katikati ya Tanzania, kaskazini mwa Somalia, kusini mwa Ethiopia na kusinimashariki mwa Sudan Kusini,” imesema taasisi hiyo huku ikiwataka wakazi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari za mapema katika kipindi hicho.
Kwa mujibu wa ICPAC, maeneo ya Kenya, Rwanda, Tanzania na Burundi zitashuhudia mvua za zaidi ya milimita 200, huku kukiwa na viwango vya juu vya joto, katika maeneo mengi ya Pembe ya Afrika.
Katika ripoti yao ya hivi karibuni, Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) na umoja wa nchi za IGAD, kwa pamoja zimesema kuwa kuna watu wapatao milioni 67 wanaokabiliwa na uhaba wa chakula katika eneo la Pembe ya Afrika.