Kwa mara ya kwanza katika historia yake, taifa la Namibia litaongozwa na mwanamke.
Hii ni baada ya matokea ya awali ya uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo, kumuonesha Netumbo Nandi-Ndaitwah akiongoza kwa kura.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Namibia (ECN), mgombea huyo kutoka chama tawala cha SWAPO, anaongoza kwa jumla ya kura 611, 989, ambayo ni sawa na asilimia 57.6 ya kura zote zilizopigwa.
Idadi ya kura hizo ni kutoka majimbo 118 kati ya 121, kulingana na ECN.
Nandi-Naitwah, ambaye ni Makamu wa Rais wa nchi hiyo, anafuatiwa na Panduleni Itula kutoka chama cha IPC, ambaye amepata kura 275, 319 (asilimia 25.9)
McHenry Venaani kutoka chama cha PDM, yuko katika nafasi ya tatu, akiwa amejikusanyia kura 54, 784 ambazo ni sawa na asilimia 5.2 huku Bernadus Swartbooi wa chama cha IPM amepata kura 51, 085, sawa na asilimia 4.8.
Uchaguzi wa Rais na wabunge nchini Namibia ulifanyika siku ya Novemba 27.