Takriban raia milioni 4.8 wameyakimbia makazi yao kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Sudan na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF), kulingana na Umoja wa Mataifa.
Kufikia Agosti 29, "takriban watu 4.8 wamekimbia makazi yao ndani na nje ya nchi kutokana na mzozo uliozuka tarehe 15 Aprili," Ofisi ya Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) ilisema katika taarifa yake.
Ilisema wakati zaidi ya watu milioni 3.8 wamehamishwa ndani, milioni moja wamevuka mpaka wa nchi yao na kuingia nchi jirani.
"Watu wamekimbia makazi yao katika majimbo yote 18," ilisema taarifa hiyo, na kuongeza kuwa karibu asilimia 72.3 ya wakimbizi wa ndani wanatoka mji mkuu Khartoum.
Mzozo mkali
Sudan imeharibiwa na mapigano kati ya jeshi na RSF tangu Aprili, katika mzozo ambao uliua zaidi ya raia 3,000 na kujeruhi maelfu, kulingana na matabibu wa ndani.
Siku ya Ijumaa, RSF ilidai kuwa iliwaua mamia ya wanajeshi wa taifa katika shambulio kwenye makao makuu ya kikosi maalum cha jeshi huko Omdurman, Magharibi mwa Khartoum, shirika la habari la Anadolu linaripoti.
Jeshi halikutoa maoni yoyote juu ya madai ya kundi la wanamgambo, lakini lilisema vikosi vyake viliendelea na mashambulizi yake yakilenga ngome za RSF kote Khartoum.
Mikataba kadhaa ya kusitisha mapigano iliyosimamiwa na wapatanishi wa Saudia na Marekani kati ya wapinzani hao wanaozozana imeshindwa kumaliza ghasia nchini humo.