Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman (kushoto) akimpongeza mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Juma Haji Duni kwa utumishi wa muda mrefu katika siasa za nchi hiyo./Picha: x.com/ACTwazalendo

Hatimaye, mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania Juma Duni Haji amestaafu siasa baada ya miongo kadhaa.

Hadi anastaafu siasa, 'Babu Duni' alikuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, tangu Januari 29, 2022, nafasi ambayo aliishika kufuatia kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 73, amewahi kushika nafasi mbalimbali za ndani ya Chama cha Wananchi (CUF); Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha Taifa, Makamu Mwenyekiti, na Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa.

Licha ya kustaafu siasa, mwanasiasa huyo mkongwe maarufu kama 'Babu Duni', atasalia kuwa kama mshauri wa Chama cha Upinzani cha ACT Wazalendo cha nchini Tanzania.

Hadi anastaafu siasa, 'Babu Duni' alikuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, tangu Januari 29, 2022, nafasi ambayo aliishika kufuatia kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad./Picha: x.com/ACTwazalendo

Safari ya 'Babu Duni' katika siasa ilianzia miaka ya 90, wakati wa vuguvugu la ukombozi wa kidemokrasia visiwani Zanzibar.

Pia atakumbukwa kwa kushiriki Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania kama mgombea mwenza wa Ibrahim Lipumba kwa mara tatu mfululizo kupitia chama cha CUF.

Mwaka 2015, 'Babu Duni' alikuwa mgombea mwenza wa Edward Lowassa katika uchaguzi wa Rais wa Tanzania kupitia tiketi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Wakati wa kuagwa kwake katika sherehe maalumu iliyofanyika Kiembesamaki, Juma Duni Haji hakuficha furaha yake ya kuona chama cha ACT Wazalendo kikiendelea kuwa imara, baada ya kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad.

“Mara baada ya kifo cha Seif, chama chetu kilipitia kipindi kigumu sana, mimi nikiwa Makamu Mwenyekiti. Tulijiuliza sana ni nani wa kurithi mikoba ya Seif, tukiamini kuwa Chama kingekufa baada ya kifo cha Seif.”

‘Babu Duni' anastaafu siasa akiacha alama isiyofichika hasa katika mapambano yake ya kudai mageuzi ya kisiasa nchini.

Katika salamu zao, kwa mwanasiasa huyo, kitengo cha vijana cha ACT Wazalendo kimesema, kuwa kimemuandalia 'Babu Duni' zawadi tatu, ambazo ni; Cheti Cha shukran, picha yenye kumbukumbu ya uongozi wake na ombi la kumtaka aandike kitabu.

TRT Afrika