Sababu ya mauaji ya Tusubira bado haijafahamika, ingawa polisi wanasema wameanza uchunguzi | Picha: Reuters

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtu aliyejihami kwa bunduki alifyatulia risasi gari la Tusubira eneo la Kyanja na kumuua papo hapo.

Tukio hilo lilitokea saa 3:20 usiku kwa saa za Uganda, wakati mwanablogu huyo alipokuwa akirudishwa nyumbani, polisi walisema.

"Taarifa za awali zinaonyesha kuwa mtu mwenye bunduki ambaye hakufahamika jina lake akiwa na bunduki aina ya SMG alilifyatulia risasi gari hilo na kusababisha kupigwa risasi kwa Ibrahim Tusubira, aliyekuwa ameketi kwenye kiti cha abiria wakati wa shambulio hilo," Naibu Msemaji wa Polisi wa Jiji la Kampala, ASP Luke Owoyesgyire, alisema kama alivyonukuliwa na gazeti la 'The Monitor'.

Sababu ya mauaji ya Tusubira bado haijafahamika, ingawa polisi wanasema wameanza uchunguzi.

"Tunawahakikishia umma kwamba kila juhudi inafanywa kuwafikisha wahusika mbele ya sheria na kutoa majibu kwa kitendo hiki cha ghasia kisicho na maana," Owoyesgyire alisema.

Tusubira, maarufu kwa jina la utani Isma Olaxess, alikuwa mwenyekiti wa Chama cha Wanablogu wa Uganda.Mwanablogu huyo hapo awali, ikiwa ni pamoja na Novemba 2021, alikamatwa na kushtakiwa kwa uchochezi.

TRT Afrika