Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amesema kuwa serikali yake haitachukua hatua zozote za kufunga mpaka au kujenga ukuta kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, kuzuia tishio kutoka kikundi cha Kigaidi cha ADF, wananaopatikana Mashariki mwa DRC, huku akisema kuwa kufanya hivyo ni sawa na kujikata kidole ili kuangamiza funza.
Kingozi huyo wa Uganda aliyasema hayo akiwahutubia wakuu wa usalama wa Uganda huku akiongeza kuwa visa vya kigaidi havitailazimu serikali yake kuharibu uhusiano bora wa raia na serikali za pande mbili.
"Nimepata mazungumzo yaliyopendekeza tufunge mpaka wa Uganda na DRC kufuatilia tukio la kigaidi la hivi majuzi, lakini sioni haja ya kufanya hivyo. NRM tutavumilia hadi tuondoe funza, lakini hatutajikata kidole ambayo ni sawa na kufunga mpaka." Museveni alisema.
Aidha, ametaja uhusiano dhaifu wa kidiplomasia kati ya Uganda na utawala wa zamani wa Kongo kwa kutoruhusu usaidizi wa kijeshi wa Uganda ili kukabiliana na ADF licha ya DRC kutokuwa na uwezo wa kuwadhibiti wanamgambo hao huku akisema kuwa hiyo iliipa ADF nguvu zaidi za kutamba mashariki mwa Kongo miaka ya awali na kuongezeka kufikia wapiganaji 2000.
Museveni ameongeza kuwa hilo pia liliiwezesha ADF kutekeleza uvamizi mbalimbali na kuzua changamoto za kiusalama zikiwemo kuvamia wanajeshi wa Kongo, na walinzi wa Umoja wa Mataifa, UN.
Hata hivyo, Rais Museveni amemsifu kiongozi wa Kongo Felix Tshisekedi kwa hatua yake ya kuwaruhusu wanajeshi wa ulinzi wa Uganda kupigana na ADF ndani ya Kongo huku akifafanua kuwa iliwaondolea changamoto za kiusalama kwa waliowaangamiza wanamgambo wa ADF na kupelekea kutawanyika kwa kikundi hicho.
Museveni amewachambua waasi wa ADF kuwa waoga waliozoea kuwalenga watu wanyonge wasio na hatia badala ya kupambana na wanajeshi wenye silaha na nguvu huku akilaani vikali uvamizi kwenye Shule ya sekondari ya Lhubirira iliyoko kando ya mpaka wa Uganda na Kongo mwezi uliopita.