Na Lulu Sanga
Katika barua yake mpya aliyochapisha kupitia ukurasa wake wa Twitter jioni ya leo, Rais huyo wa Uganda amesema kuwa alilazimika kufanya vipimo upya sababu ya safari ya kidiplomasia ambapo alipaswa kwenda kwenye upatanishi baina ya Urusi na Ukraine
"Marais wengine sita wa Afrika kutoka Comoro, Misri, Afrika Kusini, Senegal, Congo- Brazzaville na Zambia wanatarajiwa kuwasili Poland kesho kuchukua safari ya treni kuelekea Kiev ili kupatanisha vita vya Urusi na Ukraine"
Rais Museveni amesema kuwa tayari amesha wafahamisha kuwa hatojiunga nao ila ametuma muwakilishi.
"Nilipaswa kujiunga nao kesho. Sasa nimetuma ujumbe rasmi kwamba, kwa sababu ya hali yangu ya corona, siwezi kujiunga na kikundi. Dk. Rugunda atatuwakilisha. Tayari yuko Poland. Kutoka Poland, wataenda Urusi kukutana na Warusi. Nawatakia kazi njema".
Katika barua yake aliyoichapisha Twitter jumanne usiku, Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa anaendelea vyema na amerejelea kazi yake ingawa anajitenga kwa sababu bado vipimo vinaonyesha ana Uviko.
"Jumapili, Jumatatu na leo, nimekuwa nikishughulika na kazi ya karatasi. Ningekuwa nimetoka kwenye kifungo cha kibinafsi lakini tulipoangalia Jumapili, bado nilikuwa na uhakika, lakini vigezo vingine vilikuwa vyema", aliandika kupitia Twitter
Hata hivyo rais huyo amefahamisha uma kuwa mke wake mama Janeth hajambo na hajapata maambukizi ya uviko sababu wanazingatia masharti.
Aliwashukuru waliomtakia afya njema lakini akawakosoa wanaoeneza uvumi kuhusu afya yake.
"Pia niliona baadhi ya watu wachache kutoka, nadhani, Kenya, wakisema kwamba nilikuwa ICU nk. Kama ningekuwa ICU, serikali ingeijulisha nchi. Kuna nini cha kuficha? Hata hivyo, sijalala kama mgonjwa nyumbani humu isipokuwa kulala, achilia mbali kulazwa hospitali, iwe ICU au vinginevyo. Endelea kuomba, tutashinda", aliandika Museveni
Tangu kuambukizwa na virusi wa Uviko tarehe 7 Juni, Rais Museveni amekuwa akiandika barua kwa wananchi wake kupitia mtandao wa kijamii Twitter.
Lakini hakuandika tarehe 12 Juni, na hapo kupelekea watu kueneza uvumi zaidi kuwa huenda mambo si mazuri kwa afya yake.