Polisi waliwarushia vitoa machozi waandamanaji katika mji mkuu wa Kenya Nairobi mapema wiki hii. / Picha : Reuters

Kijana mwenye umri wa miaka 21 alifariki baada ya kupigwa na bomu la machozi wakati wa maandamano nchini Kenya wiki hii, afisa wa tume ya haki za binadamu alisema Jumamosi, katika tukio la pili la kifo lililotokana na maandamano yaliyoongozwa na vijana.

Wakiongozwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa Kenya ambao wamekuwa wakirusha mubashara mtandaoni matukio hayo, maandamano ya kupinga nyongeza ya ushuru yamechochewa na hali ya kutoridhika iliyoenea kuhusu sera za kiuchumi za Rais William Ruto.

Maandamano ya Alhamisi mjini Nairobi mara nyingi yalikuwa ya amani, lakini maafisa walifyatua gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha siku nzima katika jaribio la kuwatawanya waandamanaji karibu na bunge.

Kulingana na afisa wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya, Evans Kiratu mwenye umri wa miaka 21 "alipigwa na bomu la machozi" wakati wa maandamano hayo.

"Alikimbizwa hospitalini mwendo wa saa kumi na mbili jioni siku ya Alhamisi...na akafa huko," Ernest Cornel, msemaji wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya, aliiambia AFP.

"Inasikitisha kwamba kijana anaweza kupoteza maisha kwa sababu tu ya kuhangaika dhidi ya gharama kubwa ya maisha."

Mikutano hiyo ilianza jijini Nairobi siku ya Jumanne kabla ya kusambaa kote nchini, huku waandamanaji wakiitisha mgomo wa kitaifa tarehe 25 Juni.

Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Kipolisi (IPOA) ilisema Ijumaa "imeandika kifo" cha mwanamume mwenye umri wa miaka 29, "kinachodaiwa kuwa ni matokeo ya kupigwa risasi na polisi."

Utawala wa Ruto umetetea tozo zilizopendekezwa kama zinahitajika ili kujaza hazina yake na kupunguza utegemezi wa kukopa kutoka nje.

TRT Afrika